ISRAEL

Israel yaingia kwenye mgogoro wa kisiasa baada ya bunge kuvunjwa

Benjamin Netanyahu,Waziri Mkuu wa Israel
Benjamin Netanyahu,Waziri Mkuu wa Israel Sebastian Scheiner/Pool via REUTERS

Bunge la Israeli, Knesset, limevunjwa Jumanne usiku (Desemba 22) baada ya kushindwa kuidhinisha bajeti ya serikali, ikiwa ndiyo tarehe ya mwisho iliyopangwa kufanya hivyo kutokana na hali hiyo Israel imeitisha uchaguzi wa mapema utakaofanyika Machi 23 uchaguzi wa nne chini ya kipindi cha miaka miwili.

Matangazo ya kibiashara

Serikali ya umoja, iliyoundwa kufuatia makubaliano kati ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na mpinzani wake mkuu wa kisiasa Benny Gantz, haitaendelea kuhudumu mwaka ujao.

"Israeli inastahili medali ya dhahabu kwa kutokuwa na utulivu wa kisiasa," amesema mwanasayansi wa kisiasa wa Israel Yohanan Plesner, huku akimnyooshea kidole cha lawama Benjamin Netanyahu.

"Benjamin Netanyahu ndiye chanzo cha mzozo huu mpya. Hali haiwezi kamwe kuwa sawa maadamu bado yuko madarakani, " ameongeza Yohanan Plesner.

Hata hivyo baada ya bunge kuitisha uchaguzi mpya, Netanyahu alisema kuwa anaamini atashinda uchaguzi huo wa mwakani.

"Tunapinga uchaguzi, huu ni uamuzi mbaya wa Chama cha Bluu na Nyeupe, lakini ikiwa uchaguzi utalazimishwa, naahidi kwamba tutashinda," amesema Netanyahu.

Licha ya utabiri wake huo, Netanyahu mara hii atakabiliwa na hali ngumu zaidi tofauti na chaguzi zilizopita, kwani hatakuwa na uungwaji mkono wa mshirika wake Rais Donald Trump wa Marekani.