YEMENI-MAREKANI-DIPLOMASIA

Maafisa wa Marekani wakutana kwa mazungumzo na waasi wa Houthi wa Yemen

Wapiganaji wa Houthi wakipita mbele ya ubalozi wa Marekani huko Sanaa wakati wa maandamano dhidi ya Washington kwa kulichukulia kundi la waasi hao kama la kigaidi Januari 18, 2021.
Wapiganaji wa Houthi wakipita mbele ya ubalozi wa Marekani huko Sanaa wakati wa maandamano dhidi ya Washington kwa kulichukulia kundi la waasi hao kama la kigaidi Januari 18, 2021. REUTERS - KHALED ABDULLAH

Maafisa wakuu wa Marekani wameshiriki mkutano wa kwanza wa moja kwa moja na wajumbe wa waasi wa Houthi, wanaoungwa mkono na Iran ambao wanadhibiti mji mkuu wa Yemen vyanzo viwili vilivyoshiriki mazungumzo hayo vimebaini.

Matangazo ya kibiashara

Hayo yanajiri wakati utawala huko Washington unataka kupata suluhisho la mzozo wa miaka sita nchini Yemen.

Mazungumzo hayo, ambayo pande zote mbili zimeendelea kujizuia kuyaweka hadharani, yalifanyika Februari 26 nchini Oman, vyanzo hivyo vimebaini.

Mwakilishi wa Marekani kwa Yemen, Timothy Lenderking, na mjadili mkuu wa waasi wa Houthi, Mohammed Abdousalam, walihudhuria mkutano huo.

Baada ya waasi wa Houthi kuteka mji mkuu wa Yemen, Sana'a, mnamo mwaka 2014 na kudhibiti maeneo yenye idadi kubwa ya watu nchini, muungano unaoongozwa na Saudi Arabia uliingilia kati kijeshi mnamo mwaka 2015 dhidi ya waasi wa Kishia, kwa msaada wa kimyakimya kutoka nchi za Magharibi.

Mzozo huo umesababisha makumi ya maelfu ya watu kupoteza maisha na kusababisha kile Umoja wa Mataifa unachukulia kuwa mgogoro mkubwa zaidi wa kibinadamu ulimwenguni.

Saudi Arabia na waasi wa Houthi walifungua mazungumzo juu ya usitishaji wa mapigano zaidi ya mwaka mmoja uliopita chini ya mwavuli wa Umoja wa Mataifa, kwa kubadilishana wafungwa moja kwa moja.