YEMEN-SAUDIA-USALAMA

Waasi wa Houthi wadai kurusha kombora dhidi ya mitambo ya Aramco

Waasi wa Houthi nchini Yemen
Waasi wa Houthi nchini Yemen REUTERS/Khaled Abdullah

Waasi wa Houthi wa Yemen walisema Alhamisi walizindua kombora dhidi ya mitambo ya kampuni ya mafuta ya Saudi arabia Aramco, katika mji wa Jeddah kwenye pwani ya Bahari Nyekundu, shambulio ambalo mamlaka ya Saudia haijathibitisha mara moja.

Matangazo ya kibiashara

Muungano unaoongozwa na Saudi Arabia, ambao umeingilia kijeshi nchini Yemen tangu mwaka 2015, umesema umeharibu kombora la masafa marefu lililorushwa na waasi wa Houthi kuelekea Djazan, kusini mwa Saudi Arabia.

Kampuni ya Aramco, ambayo mitambo yake mikuu ya mafuta inapatikana mashariki mwa nchi, kilomita 1,000 kutoka Jeddah, haijaeleza chochote kuhusiana na shambulio hilo.

Msemaji wa wapiganaji wa kundi la waasi la Houthi amesema kuwa shambulio hilo limetokea alfajiri na limetekelezwa kwa kutumia ndege isiyo kuwa na rubani.

Akizungumza kupitia mtandao wa kijamii wa Twitter, Yahya Sarea amesema kombora hilo lilimeharibu kile walichokitaka, bila kutoa maelezo zaidi.

Shambulio kama hilo lilitekelezwa na waasi wa Houthi mwezi Novemba mwaka jana, na kuharibu kiwanda cha usambazaji cha Aramco huko Jeddah bila kuvuruga zoezi la kusafirisha mafuta kwa nchi hiyo, kulingana na kampuni hiyo kutoka Saudi Arabia.

Houthi yalenga maeneo muhimu Saudi Arabia

Waasi wa Houthi wanaendelea kutekeleza mashambulizi ya mpakani kuelekea Saudi Arabia kwa miezi kadhaa, hasa dhidi ya eneo la kusini mwa nchi. Muungano wa kijeshi unaoongozwa na Riyadh unadai kuwa uliharibu vilipuzi vingi vilivyorushwa na waasi.

Waasi wa Kishia wanaoungwa mkono na Iran mwaka jana walidai kuhusika na mashambulizi kwa kutumia ndege zisizo kuwa na rubani dhidi ya mitambo kadhaa vya kampuni ya Aramco, ikiwa ni pamoja na mtambo mkubwa zaidi wa usindikaji wa mafuta ghafi duniani.

Kwa kujibu, muungano huo ulifanya mashambulio ya angani dhidi ya eneo linaloshikiliwa na waasi wa Kihouthi.