LEBANONI

Hali ya wasiwasi yatanda Lebanon

Kwenye eneo la Mashujaa, huko Beirut, waandamanaji wakichoma matairi kwa moto na kuzuia barabara
Kwenye eneo la Mashujaa, huko Beirut, waandamanaji wakichoma matairi kwa moto na kuzuia barabara © RFI/Noé Pignède

Waandamanaji wenye hasira wamefunga barabara kadhaa nchini Lebanon leo Jumatatu kwa kutumia matairi waliochoma moto kwa siku ya saba mfululizo baada ya zaidi ya mwaka mmoja wa mdororo wa kiuchumi na miezi saba ya mgogoro wa kisiasa.

Matangazo ya kibiashara

Tangu kuanguka kwa pauni ya Lebanon Jumanne ya wiki kwa kiwango cha chini kabisa, watu wameendelea kuweka vizuizi barabarani kila kukicha.

"Tumesema mara kadhaa kuwa tuahamasisha kwa wingi maandamano kwa sababu serikali haifanyi chochote," amesema Pascale Nohra, mmoja wa waandamanaji huko Jal al-Dib.

Siku ya Jumatatu, barabara kuu tatu zinazoelekea mji mkuu kutoka miji ya Zouk, Jal al-Dib na Dora zimefungwa, na katika mji wa Beirut, waandamanaji wamefunga barabara kwa muda mfupi mbele ya benki kuu.

Rais Michel Aoun aonya waandamanaji

Mtu mmoja pia amejaribu kujiuwa kwa moto huko Tiro, lakini polisi wameingilia kati kwa wakati na kuweza kumkamata wakati akipaka mwili wake petroli, shirika la habari la serikali limeripoti.

Maafisa wa usalama na jeshi hawataruhusu kuwekwa vizuizi barabarani kwa minajili ya kulinda usalama wa raia na waandamanaji, rais Michel Aoun amejibu leo Jumatatu katika taarifa iliyotolewa baada ya mkutano na Kaimu Waziri Mkuu wa Hassan Diab na maafisa wakuu kadhaa wa usalama na fedha.

Lebanon inaendelea kukumbwa na maandamano makubwa tangu mgogoro wa kifedha wa mwaka 2019, ambao ulisababisha makumi ya maelfu ya ajira kukosekana, kufungwa kwa akaunti za benki na raia kuanza kukumbwa na njaa.

Kaimu Waziri mkuu atishia kujiuzulu

Waziri Mkuu Hassan Diab alijiuzulu lakini mrithi wake mteule Saad Hariri, aliyeteuliwa mnamo mwezi Oktoba, bado ameshindwa kuunda serikali mpya kwa sababu ya kutokubaliana na rais Michel Aoun.

Hassan Diab, ambaye anakaimu wadhifa huob siku ya Jumamosi alitishia kusitisha majukumu yake ili kuwashinikiza wanasiasa kuunda serikali mpya.