IRAN

Nyuklia: Paris, London na Berlin zashutumu tabia ya Iran

Kituo kikubwa cha nyuklia cha Natanz, Iran.
Kituo kikubwa cha nyuklia cha Natanz, Iran. - Satellite image ©2021 Maxar Technologies/AFP/File

Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zimeelezea "wasiwasi wao mkubwa" juu ya nia ya Iran ya kuongeza urutubishaji wa uranium hadi 60% katika kituo chake cha nyuklia cha Natanz.

Matangazo ya kibiashara

"Sisi, serikali za Ufaransa, Ujerumani na Uingereza (E3), tumepokea kwa wasiwasi mkubwa tangazo la Iran kwa shirika la kimataifa la kudhibiti nishati ya nyuklia (IAEA) Aprili 13 kuhusu uzinduzi wa urutubishaji wa uranium kwa 60% kwa kutumia teknolojia ya hali ya juu," nchi hizo tatu zimesema katika taarifa.

Ufaransa, Ujerumani na Uingereza zinasema zimehuzunishwa na matangazo "ya kusikitisha hasa wakati ambapo washiriki wote katika mkataba wa mwaka 2015, JCPOA na Marekani wameanza mazungumzo makubwa kwa lengo la kupata suluhisho la kidiplomasia litakalowezesha kufufua mkataba wa nyuklia wa Iran ".

Mkataba wa mwaka 2015, JCPOA, ulifikiwa kati ya Iran na wanachama watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ikiwemo Ufaransa, wanaojulikana kama “P5+1.