ISRAELI

HRW yaishtumu Israeli kwa uhalifu wa "ubaguzi wa rangi" dhidi ya Wapalestina

Bendera ya Palestina inaning'inia juu ya mti wakati wa maandamano dhidi ya makazi ya Wayahudi katika kijiji cha An-Naqura karibu na Nablus, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israeli, Machi 29, 2021.
Bendera ya Palestina inaning'inia juu ya mti wakati wa maandamano dhidi ya makazi ya Wayahudi katika kijiji cha An-Naqura karibu na Nablus, katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Israeli, Machi 29, 2021. REUTERS - RANEEN SAWAFTA

Shirika la kimataifa la Haki za Binadamu la Human Right Watch katika ripoti iliyochapishwa leo Jumanne imeishutumu Israeli kwa kufuata sera za ubaguzi wa rangi na mateso dhidi ya Wapalestina - na dhidi ya Waarabu wachache - ikiwa ni uhalifu dhidi ya binadamu.

Matangazo ya kibiashara

Shirika hilo lisilo la kiserikali lenye makao yake mjini New York limesema waraka huo haukukusudia kulinganisha taifa hilo la Kiyahudi na enzi za ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini bali ni kuchunguza ikiwa "vitendo na sera maalum" vinahusiana na ubaguzi wa rangi kama ilivyoainishwa na sheria ya kimataifa.

Israel yatupilia mbali madai ya HRW

Wizara ya mambo ya nje ya Israeli imelaani kile ilichokiita madai ya "ujinga na uwongo". Imelishutumu shirika la HRW kwa kufanya "ajenda inayopinga Israeli", ikisema kuwa shirika hilo kwa miaka mingi limekuwa "likitetea makundi ya watu wanaopinga na kususia Israeli".

Ripoti hiyo inakuja wiki chache tu baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) kutangaza kuwa imefungua uchunguzi wa uwezekano wa uhalifu wa kivita uliofanywa katika Ukingo wa Magharibi na Ukanda wa Gaza, ikitaja jeshi la Israeli na makundi yenye silaha vya Palestina kama wahusika wa uhalifu huo.

Katika ripoti hiyo, HRW inataja vizuizi vilivyowekwa na Israeli juu ya harakati za Wapalestina na maeneo yanayokaliwa kama mifano ya hatua ambazo shirika hilo linaona kama ni uhalifu wa ubaguzi wa rangi na mateso.