AFGHANISTAN

Taliban yavamia wilaya moja kaskazini mwa Afghanistan

Askari wa Marekani na Afghanistan wakipeana mikono wakati wa hafla ya kukabidhiana kambi ya jeshi ya Antonik katika mkoa wa Helmand.
Askari wa Marekani na Afghanistan wakipeana mikono wakati wa hafla ya kukabidhiana kambi ya jeshi ya Antonik katika mkoa wa Helmand. - Afghanistan's Ministry of Defence office/AFP

Wapiganaji wa Kiislamu wa kundi la Taliban, walioanzisha mashambulizi kabambe, sambamba na kuanza kwa zoezi la kuondoka kwa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan, wamedhibiti wilaya moja kaskazini mwa nchi hiyo, na kusababisha vikosi vya serikali kuondoka na kwenda mji mkuu wa mkoa wa Baghlan, maafisa wa Afghanistan wamesema leo Jumatano.

Matangazo ya kibiashara

Wapiganaji hao wa Kiislamu wamedhibiti wilaya ya Barka baada ya masaa kadhaa ya mapigano dhidi ya vikosi vya serikali, amesema Jawed Basharat, msemaji wa polisi wa mkoa, akibaini kwamba Taliban imepata hasara kubwa.

Afisa mwandamizi katika idara za usalama amesema angalau wanajeshi 10 wa Afghanistan wameuawa na wengine 16 wmetekwa na Taliban.

Rais wa Marekani Joe Biden alitangaza katikati ya mwezi wa Aprili kwamba wanajeshi wa Marekani wataanza kuondoka Afghanistan Mei 1 na kwamba wanajeshi takriban 2,500 ambao bado wako nchini humo watarudishwa Marekani Septemba 11.