UFARANSA-USALAMA

Maandamano ya kuunga mkono Wapalestina kupigwa marufuku Paris

Maandamano ya Wapalestina, hapa ilikuwa katika mji wa Chicago, Illinois, Marekani, Mei 12, 2021.
Maandamano ya Wapalestina, hapa ilikuwa katika mji wa Chicago, Illinois, Marekani, Mei 12, 2021. JBING via REUTERS - JBING

Waziri wa Mambo ya Ndani Gérald Darmanin amemuomba mkuu wa polisi katika mji wa Paris kupiga marufuku maandamano ya kuunga mkono raia wa Palestina yaliyopangwa kufanyika Jumamosi katika mji mkuu huo, kwa sababu ya "machafuko makubwa yanayoweza kuhatarisa usalama kama yale yalitotokea mwaka 2014".

Matangazo ya kibiashara

"Nimemuomba mkuu wa polisi katika mji wa Paris kupiga marufuku maandamano yanayopangwa kufanyika Jumamosi kuhusiana na mivutano ya hivi karibuni katika Mashariki ya Kati",  Waziri wa Mambo ya Ndani ameandika ujumbe kwenye Twitter, akimaanisha maandamano yaliyopangwa kufanyika Jumamosi saa 9:00 ALAASIRI huko Barbès.

Kwingineko nchini Ufaransa, "maagizo yametolewa kwa wakuu wa mikoa kuwa waangalifu na wenye msimamo," ameongeza Bw. Darmanin. "Machafuko makubwa yaliyohatarisha usalama yalishuhudiwa mwaka 2014," amebaini.

Hamas na Israel wameendelea kurushiana roketi na makombora ya angani, huku machafuko ya Wayahudi na Waarabu yakienea kote Israel.

Mzozo huo ambao umeingia siku yake ya nne leo haujaonyesha dalili za kupungua na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kampeni hiyo ya kuishambulia Gaza itachukua muda.