ISRAELI-PALESTINA

Jeshi la Israel laangusha jengo linalotumiwa na mashirika ya Habari katika ukanda wa Gaza

Jengo la Jala lililoshambuliwa na jeshi la Israel katika ukanda wa Gaza Mei 15 2021
Jengo la Jala lililoshambuliwa na jeshi la Israel katika ukanda wa Gaza Mei 15 2021 MAHMUD HAMS AFP

Jengo linalotumiwa na mashirika ya Habari ya Al Jazeera na Associated Press katika ukanda wa Gaza, limeshambuliwa na kuharibiwa na ndege za kivuta za Israeli.

Matangazo ya kibiashara

Jeshi la Israel limesema kuwa, lililazimika kuangusha jengo hilo kwa kile ilichoeleza kuwa lilikuwa linatumiwa na kundi la Hamas.

Katika hatua nyingine, Jeshi la Israeli, limeendelea kushambulia ukanda wa Gaza kwa siku ya tano mfululizo, huku mashambulizi hayo yakilenga kambi ya wakimbizi na kusababisha vifo vya Wapalestina 10, wakiwemo watoto wanane.

Inahofiwa kuwa huenda idadi ya watu waliopoteza maisha ikiwa kubwa kufuatia maafisa wa uokoaji kutoa miili zaidi katika vifusi vya majengo katika kambi hiyo  ya wakimbizi siku ya Jumamosi.

Kundi la Hamas linalodhibiti ukanda huo wa Gaza, nalo limerusha maroketi kadhaa katika miji ya Askhelon Ashdod Kusini mwa Israel lakini hakuna maafa yoyote yaliyoripotiwa.

Watu zaidi 140 wakiwemo watoto 40 wameuawa katika makabiliano hayo yanayoendelea katika ukanda wa Gaza tangu siku ya Jumatatu huku Waisrali wanane nao wakipoteza maisha.

Umoja wa Mataifa unasema Wapalestina 10,000 wameyakimbia makwao toka siku ya Jumatatu mashambulizi yalipoanza.

Wakati hayo yakijiri, mjumbe wa maalum wa Marekani Hady Amr, amewasili jijini Tel Aviv kwa mazungumzo na uongozi wa Israeli, Palestina na Umoja wa Mataifa kutafuta suluhu ya kusitisha makabiliano hayo.

Siku ya Jumamosi Wapalestina wanaandhimisha kumbukumbuku ya watu zaidi ya 700, 000 waliondolewa katika makaazi yao wakati wa vita vya mwaka 1948 wakati wa kuundwa kwa taifa la Israeli.