ISRAELI-PALESTINA

Gaza: Guterres asikitishwa na mashambulizi ya Israel dhidi ya vyombo vya habari

Jengo la al-Jalaa ambalo lina ofisi za mashirika ya kimataifa ya habari ya Associated Press (AP) na Al Jazeera limelengwa na shambulio la angani la Israeli huko Gaza, Mei 15, 2021.
Jengo la al-Jalaa ambalo lina ofisi za mashirika ya kimataifa ya habari ya Associated Press (AP) na Al Jazeera limelengwa na shambulio la angani la Israeli huko Gaza, Mei 15, 2021. REUTERS - STRINGER

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres "amesikitishwa sana na uharibifu uliosababishwa na shambulio la angani la Israeli dhidi ya jengo kubwa katika Jiji la Gaza ambalo lilikuwa na ofisi kadhaa za mashirika ya habari ya kimataifa na pia makazi ya watu," amesema msemaji wake Stéphane Dujarric katika taarifa.

Matangazo ya kibiashara

"Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza na kuzikumbusha pande zote kujiepusha na mashambulizi yanayowalenga raia na vyombo vya habari akisema yanakiuka sheria za kimataifa na kwamba ni lazima yaepukwe kwa kila hali," ameongeza pia.

Vurugu zinaendelea kati ya Israeli na kundi la Hamas linalotawala katika Ukanda wa Gaza hali inayosababisha wasiwasi katika eneo zima la Mashariki ya Kati.

Ndege za kivita za Israeli zilipiga majengo kadhaa na barabara katika sehemu muhimu ya jiji la Gaza mapema siku ya Jumapili.

Taarifa ya wizara ya afya imefahamisha kwamba watu wengine wawili wameuawa kwenye mashambulio ya hivi karibuni ambapo pia watu 25 wamejeruhiwa, ikiwa ni pamoja na watoto na wanawake.

Wakati huo huo, nyumba ya kiongozi wa kundi la Hamas ilipigwa bomu Jumapili alfajiri na majeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza huku kundi hilo nalo likiripotiwa kufyatua makombora yaliyoelekezwa katika mji wa Tel Aviv. Kiongozi huyo Yehya Al-Sinwar, ameliongoza kisiasa na kijeshi kundi la wapiganaji wa Hamas katika Ukanda wa Gaza tangu mwaka 2017.