ISRAELI-SIASA

Netanyahu ajaribu kuzuia kuondolewa kwake madarakani nchini Israeli

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu akivaa barakoa baada ya kupokea chanjo dhidi ya COVID-19 katika Kituo cha afya cha Sheba huko Ramat Gan, Israeli Desemba 19, 2020.
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu akivaa barakoa baada ya kupokea chanjo dhidi ya COVID-19 katika Kituo cha afya cha Sheba huko Ramat Gan, Israeli Desemba 19, 2020. REUTERS - Amir Cohen

Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu anatafuta njia ya kuwazuia wapinzani wake kufikia makubaliano ya kumtoa mamlakani, yaliyowasilishwa na vyombo vya habari nchini  Israeli kama mkakati mkubwa unaoendelea.

Matangazo ya kibiashara

Yair Lapid, kutoka mrengo wa kati, ana hadi Jumatano kujaribu kuunda serikali ya mseto na kulingana na vyombo vya habari nchini Israel, yuko karibu na makubaliano na vyama vya mrengo wa kushoto na kulia, hasa chama cha Yamina cha Naftali Bennett.

Naftali Bennett, 49, kiongozi mwenye ushawishi mkubwa katika mrengo wa kulia, yuko tayari kukubali pendekezo la Yair Lapid lakini bado hajawashawishi wanachama wake sita wa Bunge (Knesset) kukubali kuunga mkono kile upinzani unaita "serikali ya mabadiliko".

Kukosekana kwa idadi kubwa iliyo wazi mwishoni mwa uchaguzi wa Machi 23, muungano kama huo unaonekana kuwa dhaifu na unahitaji, ili kuweza kutawala, uungwaji mkono wa wabunge Waisraeli kutoka jamii ya Kiarabu, ambao ni nguzo za kisiasa mbali na chama cha Naftali Bennett.

Ili kuondoa mpango huu, Benjamin Netanyahu, leo Jumapili amependekeza kuanzishwa kwa serikali ya mrengo wa kulia yenye mpango wa watu watatu kushikilia nafasi ya waziri mkuu katika muhula wote mzima.

Kulingana na rasimu ya makubaliano ya muungano huo, kiongozi wa chama cha New Horizon na kiliojitenga kutoka chama cha Likud, Gideon Saar, atateuliwa kuchukuwa nafasi ya waziri mkuu kwa kipindi cha miezi 15, kabla ya kumpa nafasi Benjamin Netanyahu kwa miaka miwili, ambaye yeye mwenyewe atamkabidhi madaraka Naftali Bennett "hadi mwisho wa muhula".

Pendekezo la Netanyahu lafutilia mbali na baadhi ya wapinzani wake

Pendekezo la mkongwe wa miaka 71 wa siasa za Israeli, ambaye amekuwa madarakani kwa miaka 12, limefutiliwa mara moja na Gideon Saar.

Naftali Bennett, ambaye anatarajia kukutana na wabunge wa chama chake, bado hajajibu.

Wapinzani wa Benjamin Netanyahu, ikiwa ni pamoja na wale walio katika kambi yake mwenyewe, wanabaini kwamba kesi ya madai ya ufisadi ya waziri mkuu inahitaji mabadiliko ykwenye nafasi ya waziri mkuu.

Ikiwa Yair Lapid atashindwa kuunda serikali, Rais Reuven Rivlin labda atalazimika kuamua kuitisha uchaguzi mpya wa bunge - ambao utakuwa uchaguzi wa tano tangu mwezi Aprili 2019 - hali ambayo Naftali Bennett anasema anataka kuepusha.