IRAN-USALAMA

Meli ya kivita ya Iran yazama katika Ghuba ya Oman baada ya kuwaka moto

Moshi ukitokea kwenye meli kubwa zaidi ya Iran katika bandari ya Jask katika Ghuba ya Oman, Iran, Juni 2, 2021.
Moshi ukitokea kwenye meli kubwa zaidi ya Iran katika bandari ya Jask katika Ghuba ya Oman, Iran, Juni 2, 2021. VIA REUTERS - WANA NEWS AGENCY

Meli kubwa zaidi katika jeshi la wanamaji la Irani, Kharg, imezama katika Ghuba ya Oman Jumatano wiki hii baada ya moto ambao chanzo chake hakijajulikana kuzuka katika meli hiyo, limeripoti shirika la habari la FARS, ambalo limebainisha kuwa wafanyakazi waliokolewa.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na televisheni ya serikali ya Iran, moto ulizuka karibu saa 2:25 usiku wa Jumatano (saa za Iran) karibu na bandari ya Iran ya Jask, ambapo meli ya kivita ilikuwa ikifanya mazoezi.

Shughuli za uokoaji zilichukua saa kadhaa lakini watu waliokuwa ndani ya meli hiyo waliweza kuokolewa, televisheni ya serikali imesema.

"Jitihada zote za kuokoa meli hiyo zilishindwa na ikazama," shirika la habar la FARS limebaini.

Mwezi Aprili, Iran iliripoti kwamba moja ya meli zake, Saviz, ililengwa katika Bahari Nyekundu.

Matukio kama hayo yamezidi katika eneo hilo tangu Rais wa Marekani Joe Biden alipoiweka  Marekani kwenye njia ya kurudi tena katika mkataba wa mpango wa nyuklia wa Iran mwaka 2015, ambayo yalilaniwa mwaka 2018 na mtangulizi wake, Donald Trump.

Israeli inachukulia mpango wa nyuklia wa Iran kama tishio kwa uwepo wake, wakati Iran inakataa kutambua uwepo wa Israeli kama taifa.