AFGHANISTAN

Afghanistan: Marekani yazindua mashambulizi ya anga kusaidia vikosi vya serikali

Afghanistan inaendelea kukumbwa na mapigano kati ya wapiganaji wa Taliban na vikosi vya serikali.
Afghanistan inaendelea kukumbwa na mapigano kati ya wapiganaji wa Taliban na vikosi vya serikali. © AFP - NOORULLAH SHIRZADA

Marekani imetekeleza mashambulio ya angani kusaidia vikosi vya serikali ya Afghanistan dhidi ya mashambulizi ya Taliban wakati majeshi ya kigeni, yakiongozwa na Marekani, yakikamilisha zoezi la kuondoka nchini Afghanistan.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa Pentagon John Kirby ameiwaambia waandishi wa habari siku ya Alhamisi kuwa mashambulizi hayo ya siku za hivi karibuni yalilenga kusaidia vikosi vya usalama vya Afghanistan, bila kutoa maelezo zaidi.

Kwa upande wake, msemaji wa Taliban, Zabihullah Mujahid, amesema shambulio lilitekelezwa Jumatano jioni katika kitongoji cha Kandahar, mji ulio kusini mwa Afghanistan, na kuwaua wapiganaji wao watatu na kuharibu magari mawili.

"Tunathibitisha shambulio hilo la angani na tunalaani vikali; ni shambulio la wazi na ukiukaji wa makubaliano ya Doha kwa sababu tulikubaliana kuwa hakutakuwa na operesheni zingine baada ya mwezi wa Mei," amesema.

"Ikiwa watafanya operesheni, basi wajiandae kwa matokeo," ameongeza.