AFGHANISTAN-USALAMA

Sheria ya kutotoka nje usiku yatangazwa Afghanistan

Msafara wa vikosi maalum vya Afghanistan katika jimbo la Kandahar, Julai 13, 2021.
Msafara wa vikosi maalum vya Afghanistan katika jimbo la Kandahar, Julai 13, 2021. REUTERS - DANISH SIDDIQUI

Afghaistan ambayo inakabiliwa na mashambulizi ya Taliban kwa kipindi cha miezi miwili , sheria ya kutotoka nje usiku imetangzwa na mamlaka ya nchi hiyo. Sheria ambayo itaanza kutumika kuanzia leo Jumamosi  saa nne usiku hadi saa 10 Alfajiri nchini kote, isipokuwa majimbo matatu.

Matangazo ya kibiashara

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Afghanistan imebainisha Jumamosi hii, Julai 24, sheria ya kutotoka nje usiku imetangazwa katika mikoa 31 ya nchi, "ili kuzuia vurugu na kupunguza harakati za Taliban".

Sheria hiyo itaanza kutumika kuanzia saa nne usiku hadi saa kumi Alfajiri, bila ya kupunguzwa kwa muda katika matumizi yake. Mikoa ya Kabul, Panchir na Nagarhar haihusiki na sheria hiyo.

Kwa mujibu wa idara ya Usalama ya Afghanistan ikihojiwa na mwandishi wetu huko Kabul, Sonia Ghezali, lengo la sheria hiyo ni kuzuia Taliban kuendesha harakati zake usiku na kutumia giza ili kuiba silaha, risasi, chakula, kujificha katika maeneo ya kimkakati ili kuwa na nafasi nzuri katika mapigano na vikosi vya serikali.

Kwa sasa Taliban ina nafasi nzuri katika mapigano yanayoendelea kwani , tayari imedhibiti maeneo makubwa ya vijijini, lakini pia maeneo muhimu ya mipakani na nchi jirani (Iran, Tajikistan, Pakistan, Turkmenistan), ispokuwa tu mabarabara kuu zinazounganisha miji mikubwa ya mkoa ambazo bado ziko chini ya udhibiti wa serikali.