Michezo

Patashika nguo kuchanika nusu fainali ya Pili UEFA leo, Real Madrid dhidi ya FC Barcelona

Zikiwa zimesalia saa chache kabla ya miamba ya soka nchini Uhispania kukutana katika nusu fainali ya pili ya klabu bingwa barani Ulaya kati ya FC Barcelona na Real Madrid homa ya mpambano huo imeendelea kupanda huku Madrid wakisikitishwa na uamuzi wa UEFA kutupilia mbali madai ya klabu hiyo dhidi ya wachezaji wa Barca.

Kocha wa klabu ya Real Madrid Josee Mourinyo akitoka nje ya uwanja.
Kocha wa klabu ya Real Madrid Josee Mourinyo akitoka nje ya uwanja. AFP
Matangazo ya kibiashara

Mchezo huo ambao utapigwa katika dimba la Nou Camp unatarajiwa kuwa mkali na wakusisimua kwa muda wote wa mchezo hasa kutokana na mchezo wa awali kushuhudia Barca wakiibuka na ushindi mnono wa mabao mawili kwa bila dhidi ya Madrid.

Siku ya jana kocha Josee Mourinyo alikataa katakata kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na mchezo wake huo ambapo atashuhudia timu yake ikicheza huku yeye na wachezaji wake wawili wakiwa kwenye jukwaa la mashabiki.

Kocha wa FC Barcelona Pep Guardiola amesema kuwa anaamini vijana wake watafanya uzuri katika mchezo huo akijinasibu kuwa anakikosi bora cha wachezaji ambao ni wanasoka bora duniani.

Katika hatua nyingine shirikisho la soka barani Ulaya UEFA limetupilia mbali malalamiko ya klabu ya Madridi dhidi ya Barca kuhusiana na wachezaji wake kujiangusha muda mwingi mchezo.