UHISPANIA

Barcelona yatwaa ubingwa wa La Liga

Mashabiki wa Barcelona wakishangilia ubingwa wao wa tatu mfululizo wa La Liga baada ya mchezo wao dhidi ya Levante
Mashabiki wa Barcelona wakishangilia ubingwa wao wa tatu mfululizo wa La Liga baada ya mchezo wao dhidi ya Levante Reuters

Klabu ya Barcelona imefanikiwa kuweka rekodi ya kuwa mabingwa wa Ligi nchini Uhispania La Liga kwa mara tatu mfululizo baada ya kufanikiwa kupata pointi moja katika mchezo wao dhidi ya Levante na hivyo kukamilisha safari yao ya ubingwa kwa kuwa na pointi 92.

Matangazo ya kibiashara

Barcelona imesaliwa na michezo miwili kabla ya kumaliza Ligi msimu huu lakini tayari imeshaweka kibindoni pointi 92 ambazo zinaweza kufikiwa na Real Madrid ambayo haiwezi kutwa ubingwa kutokana na kufungwa walipokutana katika michezo yao ya Ligi.

Rekodi hii inawekwa kwa mara nyingine baada ya kushuhudiwa mara ya mwisho mwaka 1993 wakati Barcelona ikiwa chini ya Johan Cruyff ilipofanikiwa kutwaa ubingwa wa La Liga.

Katika mchezo huo Barcelona ilipata goli la kuongoza lililofungwa na Kiungo wa Kimataifa wa Mali, Seydou Keita katika dakika ya 27 ambalo lilitosha kuwapa ubingwa wa msimu huu.

Goli hilo lilidumu hadi dakika ya 40 ambapo Levante walisawazisha kupitia Mshambuliaji wa Kimataifa wa Ecuador Felipe Caicedo lakini halikuweza kuwa kizuizi kwa Barcelona kushindwa kutwaa Ubingwa wa La Liga.

Kiungo wa Kimataifa wa Uhispani na Nahodha Msaidizi wa Barcelona Xavi Hernandez amekiri kufurahishwa na ubingwa huo na amesema watafurahi pamoja na mashabiki wao kwa usiku mzima.

Naye Kocha Mkuu wa Barcelona Pep Guardiola ambaye ameshinda ubingwa wa La Liga kwa misimu yote mitatu aliyoinoa timu hiyo amenukuliwa akisema kushindwa ubingwa huwa ni kazi ngumu lakini wameweza kufanikisha hilo.

Kitu cha kupendeza kwa mashabiki wa Barcelona ni kumuona beki wa kushoto wa Kimataifa wa Ufaransa Eric Abidal akianza kwenye kikosi cha timu hiyo kwa mara ya kwanza tangu kati kati ya mwezi March.

Macho ya Barcelona kwa sasa ni kwenye mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya UEFA ambapo watakuwa na kibarua katika dimba la Wembley dhidi ya Manchester United tarehe 28 ya mwezi May.