UINGEREZA

Dalglish atwaa nafasi ya Ukocha wa kudumu katika Klabu ya Liverpool

Makao makuu ya Klabu ya Liverpool ya Uingereza
Makao makuu ya Klabu ya Liverpool ya Uingereza Reuters

Kenny Dalglish amechaguliwa kuwa Kocha Mkuu wa Klabu ya Liverpool “Vijogoo vya Jiji” baada ya kusaini mkataba wa miaka mitatu kuifundisha timu yake hiyo ya zamani ambayo aliitumika akiwa mchezaji kwa kipindi kirefu. 

Matangazo ya kibiashara

Dalglish ambaye anaonekana kama mkombozi wa Liverpool tangu achukue nafasi ya Roy Hodgson ambaye alitimuliwa baada ya mwenendo wa klabu hiyo kuwa si wa kuvutia atakuwa na kibarua cha kuhakikisha anashinda taji msimu ujao.

Steve Clarke ambaye naye yupo katika jopo la makocha wa Liverpool ambaye alikuja sambamba na Dalglish naye ameingia mkataba wa miaka mitatu ya kuendelea kurudisha heshima ya klabu hiyo ambayo tangu mwaka 1992 haijatwaa Ubingwa wa Ligi Kuu nchini Uingereza.

Mmiliki wa Klabu ya Liverpool raia wa Marekani John Henry amemsifia Dalglish kwa kazi ambayo ameifanya huku akisema anaamini ataisaidia timu hiyo kupata mafanikio zaidi.

Henry ameongeza tangu Dalglish aanze jukumu la kuinoa Liverpool mwezi January kumeshuhudiwa mapinduzi makubwa kutokana na yeye kuwa kiongozi imara na mwenye uwezo wa kutekeleza kazi zake.

Dalglish baada ya kusaini mkataba wa kuinoa Liverpool kwa miaka mitatu amesema wakati anaichukua timu hiyo lengo lake lilikuwa ni kuisaidia kutoka katika msimu mbaya lakini sasa uongozi umeona ni bora achukue jukumu hilo na kuleta mafanikio.

Wakati Dalglish anachukua jukumu hilo Liverpool ilikuwa pointi nne tu juu ya eneo la timu zinazoshuka daraja lakini sasa imejikita katika nafasi ya tano na tayari imeshakata tiketi ya kushiriki Kombe la UEFA.

Dalglish alijiunga na Liverpool mwaka 1977 akiwa mchezaji na kuweza kushinda mataji matatu ya Kombe la Europa Ligi UEFA huku pia akiweka kibindoni mataji kadhaa ya Uingereza.