ARGENTINA-RIVER PLATE

Mashabiki wa timu ya River Plate nchini Argentina wapambana na Polisi, 25 wajeruhiwa

Mashabiki wa timu ya River Plate wakipambana na Polisi nchi ya uwanja wa River's Monumental
Mashabiki wa timu ya River Plate wakipambana na Polisi nchi ya uwanja wa River's Monumental © Reuters

Zaidi ya mashabiki 25 wa timu ya River Plate ya nchini Argentina wamjeruhiwa kufuatia mapambano baina ya polisi na mashabiki hao mara baada ya kumalizika kwa mechi kati yao na timu ya Belgrano de Cordoba.

Matangazo ya kibiashara

Polisi walilazimika kutumia maji ya kuwasha na mabomu ya machozi kuwatawanya maelfu ya mashabiki wa River Plate ambao walianza kufanya fujo mara baada ya kushuhudia timu yao ikilazimishwa sare ya bao moja kwa moja na Belgrano na hivyo kushuka daraja.

Katika mchezo huo ambao River Plate walihitaji ushindi wa mabo mawili na zaidi ili kuweza kujihakikishia nafasi ya kubakia katika ligi kuu ya nchini humo, ilijikuta ikilazimishwa sare ya bao 1-1 na kuifanya kushushwa daraja msimu huu.

Mchezo huo ambao ulifanyika katika uwanja wa River's Monumental ulishuhudiwa ukimalizika katika dakika za mwisho baada ya mashabiki wa River Plate kuanza kufanya fujo kwa kurusha miale ya moto uwanjani na kurusha chupa uwanjani wakipinga matokeo hayo.

Polisi walianza kwa kurusha maji ya kuwasha katika jukwaa la mashabiki wa River Plate ambao walikuwa wakifanya fujo na kulazimu wachezaji wa timu zote mbili kusindikizwa kwenye vyumba vyao chini ya ulinzi mkali.

Zaidi ya Askari 2000 walitawanywa kabla ya mechi kufuatia uwepo wa tishio la kuzuka kwa vurugu baada ya mechi.

Viongozi wa chama cha soka nchini Argentina wanatarajiwa kukutana hii leo kujadili vurugu hizo ikiwemo hatua za kuchukuliwa dhidi ya mashabiki wa klabu ya River Plate.