Football-CECAFA

Yanga watawazwa kuwa mabingwa wa CECAFA 2011

RFI, Bilali

Yanga FC walitawazwa mabingwa kombe la Cecafa Kagame Castle mwaka 2011 baada ya kuishinda watani wao wa jadi Simba FC bao 1 kwa bila katika fainali iliyochezwa mwishoni mwa juma katika uwanja wa taifa jijini Dar es salaam.

Matangazo ya kibiashara

Bao la ushindi la Yanga lilitiwa kimyani na mshambulizi Kenneth Asamoah raia wa Ghana katika kipindi cha pili, wakati wa muda wa ziada wa fainali hiyo, kupitia kichwa baada ya kupata pasi murwa kutoka kwa mshambulizi mwezake Rashid Gumbo.

Huu ni ushindi wa nne wa klabu hii ya Yanga iliyobuniwa miaka 37 iliyopita ,huku watani wao Simba wakishinda taji hilo mara sita.

Katika fainali hizi za CECAFA, vlabu hivi sasa vimekutana mara tatu,mara ya kwanza ikiwa ni mwaka wa 1975 huko Zanzibar na Yanga kuishinda Simba mabao 2 kwa bila na baadaye Simba kuishinda Yanga tena huko Zanzibar mwaka wa 1992 kwa mabao 5 kwa 4 kupitia mikwaju ya penalti.

Yanga wameshinda taji hili chini ya mkufunzi mpya Sam Timbe kutoka Uganda,kocha ambaye amekuwa na mafaniko makubwa katika mchezo huu wa kabumbu na kushinda mataji kadhaa ya CECAFA na vlabu tofauti Afrika Mashariki na Kati.

Timbe, amewahi kushinda kombe hili la Cecafa, na klabu ya Atraco ya Rwanda, Sports Villa na Polisi zote kutoka Uganda kwa vipindi tofauti na sasa Yanga,mpinzani wake kocha wa simba Moses Basena ambaye pia ni Mganda na halikadhalika naibu mkufunzi mkuu wa timu ya taifa ya Uganda Cranes, pia amewahi kushinda taji hili na klabu ya Villa sports Club ya Uganda.

Mbali na kombe hilo, Yanga wamejinyakulia Dola elfu 30 za Marekani kama mshindi wa kwanza,wakati Simba wakitia kibindoni Dola elfu 20, huku El-Mereikh ya Sudan iliyoishinda St.Georges ya Ethiopia kwa mabao 2 kwa bila ikijinyakulia Dola elfu 10 kwa kumaliza ya tatu.