UINGEREZA-SCOTLAND

Tottenham yaanza na ushindi mnono kwenye mashindano ya Europa Ligi

Klabu ya Tottenham Hotspur imeanza vyema kampeni yake ya kusaka kucheza hatua ya makundi kwenye Kombe la Europa Ligi mchezo wa awali baada ya kutoa kipigo kizito kwa Hearts.

Matangazo ya kibiashara

Tottenham ikicheza kwa kujiamini katika mchezo huo wa awali uliopigwa nchini Scotland imefanikiwa kuibuka na ushindi wa magoli 5-0 na hivyo kujiweka katika mazingira mazuri kutinga hatua ya makundi.

Mshambuliaji wa Kimataifa wa Uholanzi Rafael Van Der Vaart ndiye alikuwa wa kwanza kufungua karamu hiyo ya magoli katika dakika ya tano ya mchezo kabla ya Jermain Defoe kupachika goli la pili.

Jake Livermore ndiye ambaye alifunga goli la tatu matokeo ambayo yalidumu hadi dakika arobaini na tano za kwanza za mchezo huo zilipomalizika huku mchezo ukiwa mkali.

Kipindi cha pili Tottenham iliingia kama mbogo na kufanikiwa kupata magoli mawili zaidi kupitia kwa Gareth Bale na Aaron Lennon na hivyo kukifanya kikosi cha Harry Redknapp kuibuka na ushindi mnono.

Kikosi cha Tottenham kilishuka dimbani bila ya Kiungo wake Luka Modric ambaye anahusishwa na kuhamia Chelsea lakini hata hivyo nafasi yake ilizibwa vilivyo na Niko Kranjcar.

Katika michezo mingine Celtic walikwenda sare tasa dhidi ya FC Sion, Stoke City wakashinda goli moja kwa nunge dhidi ya FC Thun, Fulham wakashusha kipigo cha magoli 3 kwa bila mbele ya Dnipro.

Birmingham City wakalazimishwa sare tasa dhidi ya Nacional wakati Rangers wakapata kipigo cha magoli mawili kwa moja mbele ya NK Maribor, Atletico Madrid wameanza vyema kwa ushindi wa magoli mawili kwa bila dhidi ya Guimaraes.

Schalke 04 wameanza vibaya kufuatia kupata kichapo cha magoli mawili kwa bila mbele ya HJK Helsinki nao Hannover 96 wakaichakaza Sevilla kwa magoli mawili kwa moja.