UINGEREZA

Klabu ya Arsenal yasajili wachezaji wanne kujiimarisha kabla ya dirisha la usajili kufungwa

L'entraîneur français d'Arsenal, Arsène Wenger.
L'entraîneur français d'Arsenal, Arsène Wenger. Reuters

Dirisha la Usajili Barani Ulaya limefungwa rasmi usiku wa jana na kushuhudia Klabu ya Washika Bunduki Arsenal ya Nchini Uingereza ikifanikiwa kuchukua wachezaji wanne katika dakika za lala salama kwa lengo la kujidhatiti kwa mashindano inayoshiriki mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Kocha Mkuu wa Arsenal, Arsene Wenger amelazimika kuingia soko na kusaka wachezaji zaidi baada ya kuondokewa na wachezaji wake wawili mahiri Cesc Fabregas ambaye ametimkia Barcelona pamoja na Samir Nasri aliyekwenda Manchester City.

Wenger amejikuta akifanya usajili wa Mikael Arteta kutoka Everton, Andre Santos kutoka Fenerbahce, Per Mertesacker akitokea Werder Bremen pamoja na kumnasa Yossi Benayoun ambaye wamemchukua kwa mkopo kutoka Chelsea.

Usajili huu ambao umeigharimu Arsenal kitita cha £24 milioni unatajwa kufanyika kutokana na kuchagizwa na kipigo walichokipata mwishoni mwa juma lililopita kutoka kwa Manchester United kwa kuchagazwa magoli 8-2.

Wakati Arsenal ikizidi kujiimarisha kwa ajili ya mashindano wanayoshiriki lakini imepunguza mshambuliaji wake mmoja raia wa Denmark Nicklas Bendtner ambaye amejiunga na Sunderland kwa mkopo.

Tottenham nayo ilifunga dirisha la usajili kwa kumnasa kiungo wa West Ham United Scott Parker huku ikiiwekea ngumu Chelsea kumnasa Luka Modric licha ya kutenga kitita cha £40 milioni kumnasa.

Chelsea baada ya kuambulia patupu kwa Modric ikapiga hodi Liverpool na kufanikiwa kumchukua Raul Meireles kwa dau la £12 milioni wakati Klabu ikimrejesha Craig Bellamy kutoka Manchester City aliyekuwa kwa mkopo Cardiff.

Liverpool pia imemtoa kwa mkopo Joe Cole ambaye ameelekea nchini Ufaransa katika Klabu ya Lille huku Queens Park Ranger wakinunua wachezaji wawili ambao ni Shaun Wright-Phillips na Anton Ferdinand.

Klabu ya Aston Villa nayo ilitumia vyema muda huo wa lala salama na kufanikiwa kuwanasa beki Alan Hutton kutoka Tottenham na kumchukua kwa mkopo Jermaine Jenas wakati Swansea wakimnasa Rafik Halliche.

Dirisha dogo la usajili Barani Ulaya linatarajiwa kufunguliwa mwezi January ambapo klabu zinatarajiwa kutumia muda huo kujiimarisha iwapo walikumbana na majeruhi ya aina yoyote.