UINGEREZA

Manchester City yaifungia kazi Manchester United kwa kuichakaza magoli 6-1

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Nchini Uingereza Klabu ya Manchester United imeshuhudia ikipata kichapo kikali zaidi kuwahi kutokea wakiwa nyumbani katika Uwanja wa Old Trafford tangu wafungwe mwaka 1955 baada ya kuchabangwa na wapinzani wao Manchester City kwa magoli 6-1.

Matangazo ya kibiashara

Kipigo hicho kimeonekana ni shubiri kwa Kocha mkuu wa Manchester United Sir Alex Ferguson ambaye amekiri haya ni matokeo mabaya zaidi kwake kuyapata tangu ameanza kukinoa kikosi hico zaidi ya miaka ishirini iliyopita.

Ushindi ambao imeupata Manchester City umeifanya Klabu hiyo kuendelea kuongoza ligi msimu huu kwa tofauti ya pointi tano dhidi ya wapinzani wao wakubwa kutoka Jiji moja yaani Klabu ya Manchester United.

Sir Ferguson baada ya mchezo huo amewaambia wanahabari ni udhalilishaji mkubwa ambao klabu yake imeupata baada ya kukubali kipigo hicho kikubwa wakiwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Old Trafford.

Kocha huyo mwenye msimamo mkali hakusita kutupa lawama kwa wachezaji wake wakongwe kwenye safu ya ulinzi wakiwemo Rio Ferdinand na Patrice Evra kutokana na kushindwa kutumia uzoefu wao kuzuia na badala yake wakajikuta wanashambulia hali iliyowafanya waruhusu magoli zaidi.

Dalili za kipigo kwa Klabu ya Manchester United zilianza kuonekana baada ya mlinzi wake wa kati Jonny Evans kulimwa kadi nyekundu baada ya kumuangusha mshambuliaji mtukutu Mario Balotelli ambaye alikuwa anaelekea kuliona lango lao.

Sir Ferguson amesema kutolewa kwa beki huyo wa kati ndiko kulikowamaliza kwenye mchezo huo kwani wachezaji wake walishindwa kutulia wakati huo ambapo walikuwa nyuma kwa goli moja.

Kwa upande wake Kocha wa Manchester City Roberto Mancini amekiri licha ya ushindi wao lakini Manchester United itaendelea kusalia kuwa timu kubwa zaidi yao na labda hilo litabadilika iwapo wakitwaa ubingwa msimu huu.

Magoli ya Manchester City kwenye huo yalifungwa na Mario Balotteli na Edin Dzeko ambao kila mmoja alifunga magoli mawili huku mengine yakifungwa na Sergio Aguero na Davidi Silva huku goli la kufutia machozi la Manchester United liwekwa kimiani na Darren Fletcher.