New Zealand mabingwa wapya wa dunia wa Kombe la Rugby
Timu ya Taifa ya Mchezo wa rugby ya new Zealand imefanikiwa kutwa ubingwa wa dunia baada ya kuifunga Ufaransa katika mchezo wa fainali kwa alama nane kwa saba na hivyo kumaliza ukame wa kutwaa ubingwa katika kipindi cha miaka ishirini na minne.
Imechapishwa:
Katika mchezo huo mkali ambao ulikuwa unasubiriwa kwa hamu na mashabiki wa rugby ulishuhudia Ufaransa ambayo ilikuwa unabebwa vilivyo na historia ikianza vyema katika mchezo huo kabla ya New Zealand kubadili upepo.
New Zealand ambao walikuwa na safu imara ya ulinzi walionekana wakiwadhibiti wachezaji wa Timu ya Taifa ya Ufaransa huku wakiendelea kushambulia kwa kuwavizia na hatimaye wakafanikiwa kuongoza.
Wachezaji wa Timu ya Taifa ya Ufaransa walijitahidi kufurukuta lakini wakajikuta wanashindwa kuonyesha makali yao mbele ya Vijana wa New Zealand ambao walijiapiza kulinda heshima ya taifa hilo.
New Zealand ambayo ilikuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia za rugby mwaka huu imeonekana kuwafurahisha vilivyo mashabiki wa timu hiyo ambao wajitokeza kwa wingi kuishangilia muda wote wa mchezo.
Kwa ushindi huu sasa New Zealand wamefanikiwa kurejesha historia ya mwaka elfu moja mia kenda themanini na saba ambapo waliifunga Ufaransa kwenye fainali kwa jumla ya alama ishirini na tisa kwa tisa.
Mashabiki wa rugby nchini New Zealand wamejitokeza mitaani kujumuika pamoja na wachezaji wa timu yao ya taifa kushangilia ushindi ambao wameupata kwenye fainali za mwaka huu.