UINGEREZA

Mahakama ya Uingereza yawahukumu kwenda jela wanamichezo watatu wa timu ya taifa ya Kriketi ya Pakistan

Aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Kriketi ya Pakistan, Salman Butt
Aliyekuwa nahodha wa timu ya taifa ya Kriketi ya Pakistan, Salman Butt Reuters

Mahakama ya Crown Town nchini Uingereza imewahukumu kwenda jela wachezaji watatu wa timu ya taifa ya Pakistan ya mchezo wa Kriketi baada ya kuwakuta na hatia ya kupanga matokeo wakati wa mechi zake za majaribio na timu ya Uingereza mwaka jana.

Matangazo ya kibiashara

Salman Butt ambaye alikuwa nahodha wa timu hiyo wakati wa mchezo huo amehukumiwa kwenda jela miezi 30 baada ya majaji kujiridhisha kuwa alihusika moja kwa moja na kutaka kupokea rushwa na baadae kusababisha timu yake kupoteza mchezo wao.

Kwa upande wa Muhammad Asif ambaye yeye alikuwa ni Bowler amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja baada ya kukutwa na hatia ya makosa kama ya nahodha wake Salman Butt.

Katika hatua nyingine mahakama hiyo pia imemuhukumu kwenda jela miezi sita aliyekuwa kinda wa timu hiyo Muhammad Amir baada ya kumkuta na hatia ya kukubali kupanga matokeo kwa ushawishi wa nahodha wake.

Butt na Asif wote kwa pamoja wamekana mashtaka yaliyokuwa yanwakabili ambapo mawakili wao wameapa kukata rufaa dhidi ya hukumu ambayo imetolewa.

Mahakama hiyo pia imemuhukumu kwenda jela miaka miwili na miezi nane Mazhar Majeed ambaye alikuwa wakala wa wachezaji hao kwa kushiriki moja kwa moja kuwashawishi wachezaji wake kupokea rushwa.

Amir ambaye alikuwa kinda katika timu hiyo amehukumiwa miezi sita pekee baada ya yeye mwenyewe kukiri kosa la kushiriki kupanga matokeo na kutaka kupokea rushwa kwaajili ya kutekeleza azma hiyo.