LIGI KUU UINGEREZA

Tevez kuripoti mazoezini hii leo

Carlos Tevez mchezaji wa Manchester City
Carlos Tevez mchezaji wa Manchester City foot-anglais.com

Mshambuliaji mahiri wa klabu ya Manchester City, Carlos Tevez anatarajiwa kuripoti katika mazoezi ya klabu hiyo leo hii Jumatano licha ya kuwepo wasiwasi kuwa hatarejea kwa muda unaotakiwa.

Matangazo ya kibiashara

Wasiwasi huo ulitokea jana baada ya mchezaji huyo kupigwa picha akiwa anawasili nchini mwake Argentina lakini klabu ya Manchester City imesema mchezaji huyo atarejea katika kambi ya timu hiyo.

Msemaji wa Manchester City Paul McCarthy amesema kuwa Tevez amekwenda Argentina kuangalia familia yake na atarejea kuendelea na mazoezi katika timu yake.
Hata hivyo mchezaji huyo anaweza kukabiliwa na adhabu nyingine kama hatafika katika mazoezi kama ilivyopangiwa na kocha wake Roberto Mancini.

Wachezaji wengine wa kimataifa katika klabu hiyo wako katika nchi zao kwa ajili ya michezo ya kimataifa lakini Tevez alitakiwa kubaki katika klabu hiyo ili kuendelea na mazoezi maalum.

Tevez hajacheza tangu mwezi Septemba ambapo timu yake ilishinda bao 2-0 dhidi ya timu ya Birmingham katika michuano ya kombe la Carling nchini Uingereza.

Katika hatua nyingine mchezaji huyo amekubaliana na uamuzi wa klabu yake kumpa adhabu ya kukatwa mishara ya wiki nne baada kukataa kucheza mchezo baina ya timu yake na Bayern Munich katika michezo ya klabu bingwa Ulaya.