FIFA

Sepp Blatter aomba radhi, agoma kujiuzulu

Reuters

Rais wa Shirikisho la Soka la Dunia, FIFA, Sepp Blatter leo ameomba radhi kutokana na matamshi na maoni yake ambayo alitamka kuhusu hali ya ubaguzi wa rangi katika michezo. Hata hivyo Sepp Blatter amekataa kuchukua hatua ya kujiuzulu baada ya wadau wa soka kumtaka ang'oke katika kiti hicho cha urais wa FIFA.

Matangazo ya kibiashara

Blatter amesema kuwa kitendo hicho kinaumiza sana na anaendelea kuumia kwa sababu hakutegemea matokeo ya kauli hiyo na amekiri kuwa kauli hiyo hakuitoa kwa dhamira ya kuwaumiza watu.

“Unapogundua kuwa umefanya kitu ambacho si sahihi kitu unachoweza kusema ni samahani, na mimi nasema samahani kwa watu wote walioathirika na kauli yangu”, alisema Blatter.

Hata hivyo Blatter alipoulizwa kuhusu wito uliotolewa na Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron na watu wengine wa kujiuzulu alisema kamwe hatafanya hivyo.

Blatter alikaririwa akisema kuwa vitendo vya ubaguzi wa rangi katika michezo vingeweza kumalizwa kwa kupeana mikono na kusameheana.

Kauli hiyo ya Blatter imevuruga hali ya hewa nchini Uigereza ambako amekubaliwa tayari hakubaliki kutokana kile ambacho FIFA imekuwa ikilalamikiwa kuwa haikuitendea haki wakati wa mchakato wa kuchagua mwandaaji wa fainali za Kombe la Dunia za mwaka 2018.