AFCON

Soka-Kombe la mataifa bingwa barani Afrika kuanza Jumamosi Gabon na Equitorial Guinea

Makala ya 28 ya mchezo wa soka ya kuwania ubingwa wa mataifa bingwa barani Afrika yanaanza siku ya Jumamosi nchini Gabon na Equitorial Guinea.

CAF
Matangazo ya kibiashara

Mataifa kumi na sita yanashirki katika kindubwendubwe hicho kinachochezwa katika mataifa mawili jirani,huku mababe wa soka barani Afrika Misri,Afrika Kusini, Algeria,Nigeria na Cameron wakikosa kushirki katika mashindano haya baada ya kushindwa kufuzu.

Haya ndio mataifa kumi na sita yanayoshiriki katika mashindano haya na makundi yao:

Kundi A: Malabo - Equatorial Guinea, Libya, Senegal, Zambia
Kundi B: Bata - Cote d’Ivoire, Sudan, Burkina Faso, Angola
Kundi C: Libreville- Gabon, Niger, Morocco, Tunisia
Kundi D: France Ville - Ghana, Botswana, Mali, Guinea
 

Wenyeji Equatorial Guinea wanashirki kwa mara ya kwanza katika mashindano haya pamoja na Niger na Bostwana.

Wachambuzi wa soka wanaona licha ya mataifa haya kushiriki kwa mara ya kwanza ,huenda yakashangaza mashabiki wa soka barani Afrika ambao hawayapi nafasi kubwa kwa kufanya vizuri na kusonga hadi katika hatua ya mwondoano.

Katika hatua nyingine,Black Stars ya Ghana,The Elephants ya Cote Dvoire na Senegal ndizo timu zinazopewa nafasi kubwa ya kufanya vema katika fainali hizo.

Wachambuzi wa soka wanaona kuwepo kwa wachezaji wengi wa kulipwa kutoka kwa mataifa hayo wanaocheza soka ya kulipwa katika vlabu mbalimbali huko Ulaya,kutachangia pakubwa katika kuzisaidia timu hizo kufanya vizuri.

Tayari timu zote zimewasili huko Gabon na Equitorial Guinea tayari kwa ufunguzi wa fainali za mwaka 2012 za kombe la mataifa bingwa barani Afrika.

Jumamosi hii,wenyeji Equatorial Guinea watafungua kazi na Libya saa moja na nusu usiku saa za Afrika Mashariki,huku Senegal wakicheza na Zambia saa nne usiku.