UINGEREZA

Manchester City kukabiliana na Manchester United kuamua nani atakuwa Bingwa wa Ligi Kuu

Mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney pamoja na Mchezaji wa Manchester City Mario Balootelli
Mshambuliaji wa Manchester United Wayne Rooney pamoja na Mchezaji wa Manchester City Mario Balootelli Getty image AP

Ligi Kuu nchini Uingereza inatarajiwa kuendelea usiku wa leo ambalo mahasimu wawili Manchester United ambao wanaongoza ligi watakuwa kibaruani dhidi ya wapinzani wao wa jadi Manchester City ambao wanawania ubingwa wa msimu huu kwa udi na uvumba.

Matangazo ya kibiashara

Mchezo huo wa leo ndiyo unaangaliwa kama unaweza ukaamua nani anaweza kuwa Bingwa wa msimu huu kutokana na michezo mitatu kusalia kabla ya kumalizika kwa ligi ambapo tofauti baina yao imeendelea kuwa pointi tatu pekee.

Manchester United wanatarajiwa kufunga safari kueleka Dimbani Etihad kukabiliana na Manchester City ambao kama wakishinda mchezo wa leo watakwea kileleni mwa ligi hiyo na kujiweka mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa.

Kikosi cha Kocha Sir Alex Ferguson kitakuwa na wakati mgumu kwenye mchezo wa leo kutokana na kumbukumbu mbaya ya kuchabangwa magoli 6-1 kwenye mchezo wa kwanza wa ligi na hivyo watakuwa wanapigana ili kulipa kisasi.

Vijana wa Roberto Mancini nao watakuwa na hamu ya kuhakikisha wanashinda mchezo wa leo ili wajiweke kwenye nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu kwani watakuwa wanaongoza kwa tofauti ya magoli.

Kocha wa Manchester United Sir Ferguson amewaambia vijana wake iwapo watapoteza mchezo wa leo ndoto za kutwaa ubingwa kwa mara ya 20 zitakuwa zimewekwa rehani kwa hiyo amewataka kuhakikisha wanapata ushindi ili wajihakikishie ubingwa.

Kwa upande wake Mancini anasema licha ya wao kushinda mchezo wa leo kama watafanikiwa lakini anaimani bado wanamichezo miwili migumu dhidi ya Newcastle United na Queens Park Rangers na hivyo Manchester United wananafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.

Mipango ya Manchester United kuchukua ubingwa ilingiia shubiri baada ya kufungwa na Wigan Athletic kabla ya kutoka sare ya magomi 4-4 dhidi ya Everton katika mchezo uliopigwa huko Old Trafford.