UINGEREZA

Roy Hodgson apewa mkataba wa miaka minne kuinoa Timu ya Taifa ya Uingereza

Chama Cha Soka Nchini Uingereza FA kimemtangaza rasmi Kocha Mkuu wa West Bromwich Albion Roy Hodgson kuwa Kocha wa timu ya Taifa na kumpa mkataba wa miaka minne kurithi nafasi ya Fabio Capello ambaye alivunja mkataba baada ya Nahodha John Terry kunyang'anywa Unahodha kutokana na tuhuma za kufanya ubaguzi.

Kocha Mkuu Mpya wa Timu ya Taifa ya Uingereza Roy Hodgson muda mchace baada ya kuingia mkataba wa miaka minne kuinoa timu hiyo
Kocha Mkuu Mpya wa Timu ya Taifa ya Uingereza Roy Hodgson muda mchace baada ya kuingia mkataba wa miaka minne kuinoa timu hiyo
Matangazo ya kibiashara

Hodgson ametangazwa kuwa Kocha Mkuu wa Timu ya taifa ya Uingereza na kumshinda mtu ambaye alikuwa anapigiwa upatu kwa kiwango kikubwa na mashabiki, wachezaji na hata vyombo vya habari Harry Redknapp ambaye alikuwa anaonekana mrithi sahihi wa Capello.

Kocha huyo wa zamani wa Liverpool na Fulham baada ya kukabidhiwa kibarua hicho cha kuinoa Timu ya taifa ya Uingereza amesema atahakikisha anafanya vizuri kwenye Mashindano ya Kombe la Mataifa ya Ulaya na hata kushinda kutokana na kikosi imara kilichopo.

Baada ya kupewa mkataba wa miaka minne ya kuongoza Timu ya taifa ya Uingereza Hodgson akazungumza na wanahabari lakini akakataa kuweka bayana msimamo wake ya kwamba nani atamteua kuwa Nahodha wa Timu ya Taifa.

Waandishi wa Habari walitaka kujua iwapo Nahodha wa Liverpool Steven Gerrard atakabidhiwa jukumu hilo lakini akakataa kuweka bayana nani ambaye atakuwa kinara wa wachezaji ndani ya uwanja.

Hodgson pia alichelea kuweka msimamo wake juu ya kuwaita kwenye timu hiyo mabeki John Terry wa Chelsea na Rio Ferdinand ambaye anakipiga katika Klabu ya Manchester United kutokana na kutokuwa na uhusiani mzuri baina yao.

Kocha huyo akasema kuwa atamwita Wayne Rooney kwenye kikosi chake kitakachokwenda kwenye Fainali za Komba la mataifa ya Ulaya katika nchi za Poland na Ukraine licha ya kukosa michezo miwili ya kwanza kutokana na kazi nyekundu aliyopoewa kwenye hatua ya kufuzu.

Kibarua cha kwanza kwa Roy Hodgson kitakuwa michezo ya kirafiki kabla ya kueleka kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Ulaya zitakazofanyika mwezi Juni na Julai katika ardhi ya Poland na Ukraine.