UTURUKI

Chama cha soka nchini Uturuki chazisafisha baadhi ya vilabu kutokana na kashfa ya kupanga matokeo

Mashabiki wa soka nchini Uturuki
Mashabiki wa soka nchini Uturuki Reuters

Chama cha soka nchini Uturuki TFF, kimetangaza kuzisafisha baadhi ya timu zilizokuwa zinashiriki ligi kuu ya nchini humo kwa tuhuma za rushwa kwaajili ya kupanga matokeo.

Matangazo ya kibiashara

Shirikisho hilo la mpira kwenye taarifa yake limesema kuwa uchunguzi wao ulizingatia msimu wa soka mwaka 2010/2011 ambapo zaidi ya timu ishirini na mbili zilikuwa zikichunguzwa kutokana na kashfa ya kuhusika kupanga matokeo.

Miongoni mwa vlabu ambavyo vilionja joto ya jiwe, ilikuwa ni klabu ya FC Fenrebahce ambayo ilizuiwa kushiriki klabu bingwa ulaya wala EUROPA league kutokana na kutuhumiwa kupanga matokeo kwenye mchezo wao wa mwisho wa ligi ili kutwaa ubingwa.

Sakata hilo la upangaji matokeo pia linawahusisha makocha na baadhi ya wachezaji 98 ambao pamoja na vilabu vyao kufutiwa kashfa ya upangaji matokeo, uchunguzi dhidi yao bado unaendelea kubaini endapo walihusika moja kwa moja kupanga matokeo.

Mbali na kuendelea kuwahoji wachezaji na makocha, shirikisho hilo pia limewafungia wachezaji wawili baada ya kubaini kuwa walishirikia kikamilifu kupanga njama za kupanga matokeo.

Wachezaji hao ni Ibrahim Akin wa klabu ya Istanbul Buyuksehir aliyefungiwa miaka mitatu ambaye amebainika kupanga matokeo wakati timu yake ilipofungwa mabao 2-0 na klabu ya FC Fenerbahce.

Mchezaji mwingine aliyeangukiwa na rungu hilo ni Serdar Kulbilge anayekipiga na klabu ya Ankaragucu kwa miaka miwili baada ya kubainika kupanga njama za timu yake kufungwa mabao 4-2 dhidi ya Fenerbahce.