NDONDI

Pambano kati ya bondia Amir Khan na mpinzani wake Lamont Peterson laahirishwa

Mabondia Peterson na Amir Khan ambao pambano lao limeahirishwa
Mabondia Peterson na Amir Khan ambao pambano lao limeahirishwa Reuters

Pambano la ngumi la uzito wa Light-welterweight kati ya mabondia Amir Khan na mpinzani wake Lamont Peterson limeahirishwa baada ya Peterson kubainika kutumia dawa zisizofaa mchezoni.

Matangazo ya kibiashara

Pambano hilo ambalo lilikuwa limepangwa kufanyika tarehe 19 ya mwezi huu kwenye uwanja wa Las Vegas, limelazimika kusogezwa mbele baada ya bondia Peterson kubanika kutumia dawa za kuongeza nguvu kabla ya pambano.

Mabondia wote wawili walikubaliana hapo awali kufanya vipimo vya damu kabla ya pambano lao ambapo mara baada ya majibu kutoka bondia Peterson alibainika kutumia dawa hizo aina ya synthetic testosterone.

Peterson mwenyewe akihojiwa mara baada ya vipimo hivyo alikiri kutumia dawa hizo na kudai kuwa anajutia kitendo chake kwakuwa alitaka kupigana na Khan.

Khan amesema kuwa amesikitishwa na kitendo kilichofanywa na mpinzani wake wakati alijua fika kuwa hakupaswa kutumia dawa zozote kabla ya mchezo wao.

Pambano la awali lilishuhudia bondia Amir Khan akipoteza ubingwa kwa Peterson baada ya kushindwa kwa alama, kwenye matokeo ambayo Khan aliyapinga vikali na kutaka mechi ya marudiano.