TANZANIA

Twiga stars yapigwa 5-2 na Banyana Banyana

RFI

Timu ya soka ya wanawake ya Tanzania, Twiga Stars jana ilipigwa kikumbo na timu ya wanawake ya Afrika Kusini, Banyana Banyana baada ya kukubali kipigo cha mabao 5-2 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliofanyika katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

Matangazo ya kibiashara

Timu zilianza mchezo kwa umakini huku zikisomana lakini walikua ni Banyana Banyana walionza kutikisa nyavu Twiga Stars kunako dakika ya 25 ya mchezo kupitia kwa nahodha wa zamani wa timu hiyo Modise bao ambalo lilidumu hadi kipenga cha mwisho cha kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Banyana Banyana wakianza kushambulia kwa kasi na kunako dakika ya pili ya kipindi cha pili walifanikiwa kupata bao la pili hali iliyozidi kuwachanganya Twiga Stars.

Twiga Stars walifufua matumaini baada ya kupata bao la kwanza katika dakika ya 65 lililotiwa kimiani Fatuma Bashiri kwa mkwaju wa penati baada ya Banyana Banyana kupata kufanya madhambi katika eneo la hatari.

Katika dakika ya 75 Sanah Mollo alipatia timu yake ya Banyana Banyana bao la tatu lakini dakika tano baadaye Twiga Stars walipata bao la pili kupitia kwa nahodha Asha Rashid.

Banyana Banyana walipata bao la nne na bao lililohitimisha kalamu ya magoli lilifungwa na Van Wyk na kuzamisha kabisha matumaini ya Twiga Stars na hadi kipenga cha mwisho kinapulizwa Banyana Banyana 5 na Twiga Stars 2.