UFARANSA-UINGEREZA

Kiungo wa Klabu ya Lille Hazard atangaza kujiunga na Chelsea ya Uingereza

Kiungo wa Kimataifa wa Ubelgiji na Klabu ya Lille Eden Hazard atangaza kujiunga na Chelsea
Kiungo wa Kimataifa wa Ubelgiji na Klabu ya Lille Eden Hazard atangaza kujiunga na Chelsea

Mchezaji wa Kimataifa wa Ubelgiji ambaye ameng'ara katika msimu huu wa Ligi Kuu nchini Ufaransa akiwa na Klabu yake ya Lille Eden Hazard amesema anataka kujiunga na Mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya Chelsea.

Matangazo ya kibiashara

Hazard mwenye umri wa miaka ishirini na moja ambaye saini yake inawindwa kwa udi na uvumba na mahasimu Manchester United na Manchester City ameweka bayana msimamo wake kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter.

Kiungo huyo ambaye amekuwa gumzo kutokana na kiwango chake ambacho amekionesha kwenye Ligue 1 amesema anataka kwenda Stamford Bridge ambapo anaamini itakuwa sehemu muafaka kwake kisoka.

Hazard usajili wake unaweza ukagharimu kitita cha £32 milioni na kuingia mkataba wa miaka mitano kuitumika Chelsea ambayo nayo ilionesha nia ya kumsajili mshambuliaji huyo raia wa Ubelgiji ambaye kwa sasa yupo na Kikosi cha Timu ya Taifa.

Chelsea yenyewe imekataa kutoa hakikisho kama imemnasa Hazard lakini kupitia kwenye mtandao wake imesema itakuwa inatangaza usajili wake kila inapokamilisha usajili wa mchezaji ambayo wanamhitaji.

Hazard anatarajiwa kuwakilisha kikosi cha Timu ya Taifa ya Ubelgiji kwenye mchezo wao dhidi ya Uingereza ambapo watakutana kwenye mchezo wa kirafiki ambao utapigwa siku ya jumamosi.

Hazard amemaliza msimu huu akiwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu nchini Ufaransa na amekuwa mchezaji wa pili wa kigeni kuweza kushinda tuzo ya uchezaji bora kwa wachezaji wenye umri mdogo mara mfululizo ikiwa ni mwaka 2009 na 2010.

Hazard ameshaitumikia timu ya taifa ya Ubelgiji kwenye michezo ishirini na sita huku akionekana kuwa kiungo tegemeo kwa sasa kutokana na soka yake ya kuvutia ambayo amekuwa akiionesha.