UINGEREZA-UJERUMANI

Klabu ya Manchester United yakaribia kumnasa Shinji Kagawa kutoka Borussia Dortmund

Kiungo wa Kimataifa wa Japan anayekipiga katika Klabu ya Borussia Dortmund Shinji Kagawa anayewaniwa na Manchester United
Kiungo wa Kimataifa wa Japan anayekipiga katika Klabu ya Borussia Dortmund Shinji Kagawa anayewaniwa na Manchester United

Klabu ya Manchester United ya Uingereza inakaribia kukamilisha usajili wa Kiungo wa Kimataifa wa Japan ambaye anakipiga katika Klabu ya Borussia Dortmund ya Ujerumani Shinji Kagawa.

Matangazo ya kibiashara

Taarifa zilizotolewa na Mkurugenzi wa Mabingwa hao wa Ujerumani Borussia Dortmund Michael Zorc zimethibitisha kukamilika kwa mapatano baina yao na Klabu ya Manchester United na kilichosalia ni makubaliano binafsi na mchezaji.

Klabu ya Borussia Dortmund imesema makubaliano yote yameshafikiwa na sasa Manchester United wanaendesha mazungumzo taratibu na Kiungo huyo mwenye umri wa miaka ishirini na tatu kuweza kueleka Old Trafford.

Kitita kilichoafikiwa kumuamisha Kagawa kutoka Borussia Dortmund kueleka Manchester United kitakuwa ni £12 milioni na zinaweza kupanda na kufikia £17 milioni kulingana na mafanikio ambayo atayapata akiwa Old Trafford.

Kagawa amefunga magoli kumi na tatu katika mechi thelathini na moja ambazo amecheza akiwa na Borussia Dortmund ambayo imefanikiwa kutwaa makombe mawili ambayo ni Kombe la Chama Cha Soka na lile Kombe la Ligi.

Kiungo huyo wa Kimataifa wa Japan alijiunga na Borussia Dortmund akitokea Klabu ya Cerezo Osaka inayokipiga katika J-League mwaka elfu mbili na kumi kwa kitita cha euro 35,000.

Manchester United inamsaka Kagawa kwa leongo la kujiimarisha kwa msimu ujao kufuatia msimu huu kumaliza bila ya kupata kombe lolote huku wakiondolewa kwenye hatua ya makundi kwenye Mashindano ya Ligi ya Mabingwa Barani Ulaya.