Brazil 2014

Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati yaanza vibaya fainali za kufuzu kwa kombe la dunia nchini Brazil mwaka 2014

Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati yameanza vibaya safari ya kuelekea Brazil kushiriki katika fainali ya kandanda ya kombe la dunia mwaka 2014.

Matangazo ya kibiashara

Harambee Stars ya Kenya ikiwa nyumbani ilitoka sare ya kutofungana na Malawi katika uwanja wao wa nyumbani wa Moi Kasarani jijini Nairobi, mechi ambayo ilithibitiwa kwa kiasi kikubwa na vijana wa Malawi ambao waliridhika na sare waliyopata jijini Nairobi.

Nigeria ambayo pia imejumuishwa katika kundi moja na Kenya, iliishinda Namibia kwa bao 1 kwa 0 mechi waliocheza wakiwa nyumbani.

Taifa Stars ya Tanzania ililemewa na miamba wa soka barani Afrika Cote dvoire na kufungwa mabao 2 kwa 0 mjini Abidjan,huku Uganda ikilazimishja sare ya bao 1 kwa 1 na wenyeji wao Angola mjini Luanda.

Cameroon iliichabanga Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo bao 1 kwa 0, wakati Algeria ikiifunga Rwanda mabao 4 bila 0.

Mabingwa watetezi wa kombe la mataifa ya Afrika Chipolopolo ya Zambia ilijipata pabaya baada ya kukubali kipigo cha mabao 2 kwa 0 dhidi ya Sudan mjini Khartoum.

Michuano ya pili zitachezwa mwishoni mwa wiki hii.

Mataifa ya Afrika yapo katika raudi ya pili ya kufuzu kwa  fainali hizo za dunia,na mataifa 10 yatayofuzu katika awamu hii yataingia katika awamu ya tatu na ya mwisho ya kufuzu kwa fainali hizo.

Bara la Afrika litatoa mataifa 5 kushiriki katika fainali hizo mwaka 2014.