Zambia

Chipolopolo yasema itafungua uwanja mpya kwa ushindi dhidi ya Ghana Jumamosi hii

Mabingwa wa soka barani Afrika Zambia, wanasema hawawezi kupoteza mchuano wao wa kufuzu kwa kombe la dunia mwaka 2014 dhidi ya Ghana Jumamosi hii .

Matangazo ya kibiashara

Chipolopolo walichabangwa mabao 2 kwa 0 na Sudan katika mchuano wao wa kwanza jijini Khartoum mwishoni mwa juma lililopita na ikiwa watafungwa Jumamosi hii itakuwa vigumu kwao kusonga mbele katika awamu ya tatu ya kufuzu kwa fainali hiyo.

Black Stars nayo ilianza kampeni yake kwa nguvu baada ya kuisambaratisha Lesotho kwa mabao 7 kwa 0 ushindi ambao umewapa matumaini ya kusonga mbele katika kinyanganyiro hicho.

Mechi ya maruadiano itachezwa katika uwanja mpya wa Levy Mwanawasa mjini Ndola na maafisa wa soka nchini humo wana matumaini makubwa kuwa vijana wa chipolopolo watafungua uwanja huo kwa ushindi.

Mataifa ya Afrika yanashiriki katika mzunguko wa pili ya safari hii ya kwenda nchini Brazil na timu kumi bora katika kila kundi yatafuzu katika mzunguko wa tatu kabla ya timu tano bora kupatikana kuliwakilisha bara la Afrika katika fainali hizo.