TENNIS-FRENCH OPEN

Maria Sharapova na Sara Errani kumenyana katika fainali ya French Open siku ya Jumamosi

Maria Sharapova kutoka Urusi na Sara Errani kutoka Italia watamenyana katika fainali ya makala ya mwaka huu ya mashindano ya Tennis ya French Open kwa upande wa akina dada  yanayoendelea jijini Paris  Jumamosi hii .

Matangazo ya kibiashara

Sharapova anayeorodheswa wa pili duniani alitinga fainali baada ya kumchabanga Petra Kvita kutoka Jamhuri ya Czech kwa seti 2 kwa 0 za  6-3 na 6-3, huku Errani anayeorodheshwa wa 21 akimshinda Samantha Stosur kutoka Australia  anayeshikilia nafasi ya  6  duniani kwa seti za 2 kwa 1 za 7-5, 1-6, 6-3.

Sharapova ambaye amewahi kushinda taji la Wimbledon mwaka 2004 huko Uingereza, US Open nchini Marekani mwaka 2006 na 2008 anapewa nafasi kubwa ya kunyakua taji hilo dhidi ya Errani ambaye anafikia katika fainali ya michunao mikubwa kama hii kwa mara ya kwanza.

Ikiwa Sharapova ataibuka mshindi ataorodheswa katika nafasi ya kwanza kama mwanamke bora duniani na kuchukua nafasi ya Li Na kutoka nchini China aliyeshinda michuano hii mwaka uliopita na kuondolewa mapema katika kinganyiro hiki.

Kwingineko, kwa upande wa wanaume katika nausu fainali Ijumaa, Mserbia Novak Djokovic anachuana na Mswizi Roger Federer wakati David Ferrer akimaliza kazi na Rafael Nadal.

Fainali ya wanaume itachezwa Jumapili hii.