Michezo-EURO 2012

UEFA yalaani ghasia za Warsaw

Polisi wakipiga doria baada ya vurugu
Polisi wakipiga doria baada ya vurugu REUTERS/Kai Pfaffenbach

Shirikisho la soka barani Ulaya, UEFA limeshutumu ghasia zilizotokea kwenye mitaa ya mji wa Warsaw kabla ya pambano la jumanne kati ya mwenyeji mshirika wa mashindano ya Euro2012 Poland na Urussi.

Matangazo ya kibiashara

Polisi imewatia mbaroni watu 184, ikiwa ni raia 156 wa Poland na Warussi 24 kufuatia mapigano makali baina ya mashabiki ambao waliwashambulia Polisi pia.

Wakuu wa nchi walikua wamejiandaa kwa uwezekano wa mtafaruku kutokea kabla ya mchuano wa jumanne ikizingatiwa kwamba uhusiano kati ya nchi hizi mbili umetiwa sumu na migogoro ya miaka mingi ikikumbukwa pia uvamizi na utekaji wa Poland kwa kipindi cha miaka 40 baada ya vita vikuu vya pili vya Dunia.

Ghasia zilizuka wakati maelfu ya mashabiki wa Urussi wakisindikizwa na polisi walivuka mto Vistula wakiwa njiani kwenda uwanjani. Mapigano mengine yalizuka katikati ya mji katika eneo la mashabiki baada ya mechi iliyomalizika kwa sare ya bao moja kwa kila upande.