CECAFA

Timu za Tanzania zaanza vibaya mashindano ya soka ya CECAFA

Makala ya 39 ya kutafuta ubingwa wa klabu bora katika mchezo wa soka Afrika Mashariki na Kati CECAFA yanaendelea jijini Dar es salaam nchini  Tanzania.

Matangazo ya kibiashara

Kindubwendubwe hicho kilichoanza Jumamosi iliyopita, kimeanza kuzua msisimko mkubwa sana na hadi sasa mabao 20  yamefugwa katika mechi tano ambazo zimechezwa.

Wenyeji wa mashindano haya vlabu vya Yanga,Simba na Azam FC vimeanza vibaya baada ya timu hizo kukosa kuadikisha ushindi katika mechi zao za ufunguzi.

Yanga FC ya Tanzania ambao ni mabingwa watetezi walifungwa na Athletico FC ya Burundi mabao 2 kwa 0 katika mchuano wa ufunguzi, huku Simba wakilazwa na URA ya Uganda pia kwa mabao 2 kwa 0.

Azam FC ilitoka sare ya bao 1 kwa 1 na Mafunzo FC kutoka visiwani Zanzibar.

Katika matokeo mengine, APR ya Rwanda iliichabanga Wau Salaam FC ya Sudan Kusini mabao 7 kwa 0, huku Vita Club ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambao wamealikwa katika mashindano haya wakiwashinda AS Port ya Djibouti kwa mabao 7 kwa 0.

Timu 11 zinashiriki katika mashindano haya.