TANZANIA-RWANDA

Hatimaye Kombe la Kagame kubaki Tanzania kwa mara nyingine

Mashabiki wa timu ya Yanga nchini Tanzania watazamiwa kujitokeza kwa wingi katika fainali za kagame uwanja wa taifa Dar es salaam
Mashabiki wa timu ya Yanga nchini Tanzania watazamiwa kujitokeza kwa wingi katika fainali za kagame uwanja wa taifa Dar es salaam AFP

Hatimaye michuano ya kuwania kombe la Kagame ambalo limeendelea kurindima Dar es salaam nchini Tanzania inakaribia kutia nanga huku kila dalili zikionesha Kombe hilo kuendelea kubaki Tanzania baada ya timu za APR ya Rwanda na AS Vita ya DR Congo kukubali kufungashiwa virago katika mechi za nusu fainali.

Matangazo ya kibiashara

Kwa mara nyingine timu mbili kutoka Tanzania,Mabingwa watetezi Yanga wanakutana na Azam katika fainali ya Kombe la Kagame baada ya timu hizo kuzifunga APR ya Rwanda na AS Vita ya DR Congo katika mechi za nusu fainali zilizofanyika alhamisi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Yanga ilipata ushindi wake wa bao 1-0 dhidi APR kwa goli la Hamis Kiiza aliyefunga kwa kifua akiunganisha krosi ya Haruna Niyonzima, huku Azam ikiilaza AS Vita kwa mabao 2-1 mabao yaliyopachikwa kimiani na John Bocco na Mrisho Ngasa.

Kwa matokeo hayo sasa Kombe la Kagame linabaki Tanzania kwa mara ya pili mfululizo baada ya mwaka jana Yanga kucheza fainali na Simba.