SOKA

Robin van Persie asajiliwa na Manchester United

Klabu ya soka ya Uingereza Manchester United imemsajili mshambulizi wa Arsenal Robin van Persie.

Matangazo ya kibiashara

Klabu ya Arsenal ilikubali kuumuuza Van Persie kwa kima cha Pauni Milioni 24 baada ya maafikiano na Manchester United.

Mshambulizi huyo wa kimataifa wa Uholanzi mwenye umri wa miaka 29 atakumbukwa sana katika klabu ya Arsenal baada ya kuifungia klabu hiyo mabao 37 msimu uliopita.

Manchseter United ilionesha nia ya kumsajili Van Persie baada ya mchezaji huyo kusema kuwa anataka kuichezea klabu hiyo na hataki tena kuichezea Arsenal msimu huu.

Wachambuzi wa soka nchini Uingereza wanaona kuwa imekuwa busara kwa Arsenal kumuuza Van Persie badala ya kumwacha kuondoka katika klabu hiyo mwenyewe.

Van Persie alijiunga na Arsenal akiwa na miaka 20 mwaka 2004 na kujiunga kwake katika klabu ya Manchester United kumeelezwa pia na wachambuzi wa soka kuwa kutasaiadia Manchester United kunyakua taji hilo.

Joseph Marwa ni mchambuzi wa soka kutoka jijini Nairobi nchini Kenya, yeye anasema kuwa huu ndio usajili mkubwa kuwahi kufanywa na Manschster United katika misimu ya hivi karibuni na ushirikiano kati ya Van Persie na Wayne Rooney utakuwa bora zaidi katika klabu hiyo.

Aidha, Marwa anaongeza kuwa kutokana na umri wa Van Persie huenda amepata klabu ambayo atamalizia kucheza soka  na pia anatafuta kuishindia Manchester United taji baada ya kuikosoa katika klabu yake ya zamani ya Arsenal.

Msimu wa mwaka 2012/2013 wa ligi kuu ya Uingereza unaanza Jumamosi hii.