Soka

Pienaar astaafu kuichezea Bafana Bafana ya Afrika Kusini

Nahodha wa timu ya taifa ya soka Bafana Bafana Steven Pienaar anayechezea pia klabu ya Everton ya Uingereza ametangaza kujiuzulu kucheza soka la kimataifa kwa kile alichokisema kuwa mwili wake umechoka.

Matangazo ya kibiashara

Pienaar,ambaye alichukua nafasi ya Aaron Mokoena kama nahodha wa Bafana Bafana wakati wa kombe la dunia mwaka 2010 amesema amechukua uamuzi huo pia kutokana na kutoweza kuichezea klabu yake na timu ya taifa kwa wakati mmoja.

Uamuzi wa kujiuzulu kwa Pienaar umepokelewa na shirikisho la soka nchini Afrika Kusini huku kocha wa Bafana Bafana Gordon Igesund akisema amesikitishwa mno na hatua ya kujiuzulu kwa Pienaar.

Hata hivyo Igesund amesema ni sharti uamuzi wa Pienaar uheshimiwa na kupongezwa kwa kuichezea Bafana Bafana kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita na kusaidia kuinua kiwango cha soka nchini humo.

Aidha, kocha huyo ameongeza kuwa Pienaar anakaribishwa tena kuichezea Afrika Kusini ikiwa atabadilisha mawazo wakati huu timu hiyo inapojiandaa kuwa wenyeji wa mechi za kombe la mataifa bingwa barani Afrika mwaka ujao.

Bafana Bafana inajiandaa kucheza mechi ya kirafiki za kimataifa na Poland tarehe 12 mwezi huu kabla ya kusafiri hadi jijini Nairobi kucheza na Harambee Stars ya Kenya tarehe 16.