Soka

Puyol kukosa Clasico dhidi ya Real Madrid siku ya Jumapili

Barcelona itakosa huduma za nahodha wake Carles Puyol wakati wa mchuano wa ligi kuu ya La Liga nchini Uhispania kati yake na Real Madrid siku ya Jumapili katika uwanja wao wa nyumbani wa Nou Camp  baada ya kujeruhiwa.

Matangazo ya kibiashara

Puyol alijeruhiwa kiwiko cha mkono wakati wa mchuano wa Barcelona na Benfica ya Ureno Jumatano usiku , mchuano wa kuwania taji la klabu bingwa barani Ulaya mechi ambayo walishinda kwa mabao 2 kwa 0.

Kocha Tito Vilanova amethitibisha kuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Uhispania atakosa mchuano huo wa Clasico unaosubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka duniani.

Nahodha huyo anatarajiwa kupata matibabu kwa muda wa wiki nane zijazo  kabla ya kurudi tena  uwanjani  kwa mujibu wa madaktari wake.

Barcelona haijapoteza mchuano wowote tangu kuanza kwa  ligi kuu ya soka  nchini Uhispania msimu huu na kwa sasa inaongoza msururu wa ligi hiyo kwa alama 8 baada ya mechi sita ikifuatwa na Real Madrid.

Puyol amejeruhiwa tena wiki mbili baaada ya kupona jeraha lingine la goti.