Soka

Wasiwasi yaikumba Manchester City baada ya kutoka sare na Borussia Dortmund

Kocha wa klabu ya soka nchini Uingereza Manchester City Roberto Mancini amewataka wachezaji wake kuongeza jitihada na kuwa makini katika mechi zinazosalia ikiwa wanataka kufika mbali katika harakati za kuwania taji la msimu huu la  klabu bingwa barani Ulaya.

Matangazo ya kibiashara

Mancini ambaye aliongoza Manchester City kunyakua taji la klabu bingwa nchini Uingereza msimu uliopita amesema sare waliopata ya bao 1 kwa 1 dhidi ya klabu ya Borussia Dortmund kutoka Ujerumani siku Jumatano usiku wakiwa katika uwanja wao wa nyumbani ni ishara kuwa wana kazi kubwa ya kufanya.

Klabu hiyo ilipata sare hiyo, baada ya kufungwa na Real Madrid kwa mabao 3 kwa 2 katika mchuano wake wa ufunguzi mwezi uliopita.

Manchester City ndio klabu pekee barani Ulaya ambayo imetumia kitita kikubwa cha fedha kuwasajili wachezaji wapya ikikisiwa kuwa misimu minne iliyopita imetumia Euro Milioni 440 kwa usajili pekee.

Klabu hiyo kwa sasa ni ya tatu katika kundi lao kwa alama tatu, kundi linaloongozwa na Real Madrid kwa alama 6, Borussia Dortmund ni ya pili kwa alama 4 huku Ajax ikiwa ya mwisho bila ya alama yeyote.

Manchester City itakutana na Ajax FC baadaye mwezi katika mchuano wake wa tatu.