Christiano Ronaldo aonyesha uwezo, aumia bega huku timu yake ikitoka sare ya 2-2

RFI

Mchezaji wa kimataifa wa Real Madrid Cristiano Ronaldo anajiunga na timu yake ya taifa ya Ureno licha ya kuumia bega katika mechi ya jana na mahasimu wa FC Bercelona.

Matangazo ya kibiashara

Klabu yake ya Real Madrid imethibitisha hatua hiyo na kusema kuwa majeraha yake Ronaldo si makubwa sana kumzuia kujiunga na timu yake ya taifa.

Katika mchezo wa jana Real Madrid walitoka sare ya mabao 2-2 na mahasimu wa wao Barcelona katika mchezo wa ligi ya Hispania maarufu kama La Liga.

Ronaldo katika kipindi cha pili aliumia bega wakati akijaribu kufunga kwa kichwa mpira uliopigwa akiwa katika haraka za kuisaidia klabu yake.

Katika mchezo wa jana Ronaldo alifanikiwa kuifungia timu yake mabao yote mawili wakati Lionel Messi naye aliifungia timu yake ya Barcelona.

Klabu ya Real Madrid imesema kuwa tayari imelifahamisha Shirikisho la Soka la Ureno kuhusu hali ya mchezaji huyo nguli kwani bada ya kufanyiwa uchunguzi na madaktari imeonekana hana madhara makubwa.

Kwa sasa Ronaldo anabaki katika uangalizi wa madaktari na anatarajiwa kuonekana viwanjani katika michezo ya kuwania kufuzu kucheza fainali za Kombe la Dunia ijumaa wiki hii wakati timu yake itacheza ugenini ikibiliana na Urusi.

Siku nne baadaye timu yake ya Ureno itashuka dimbani kumenyana na Ireland Kaskazini katika mchakato huohuo.