KENYA-AFRIKA KUSINI

Bafana Bafana yachekelea mechi na Harambee Stars

RFI

Shirikisho la Soka la Afrika Kusini, SAFA limeeleza kuvutiwa kwake na mchezo wa kirafiki kimataifa ambao timu ya taifa ya soka ya nchi hiyo, Bafana Bafana itakabiliana na timu ya taifa ya Kenya Harambee Stars.

Matangazo ya kibiashara

Rais wa SAFA Kirsten Nematandani amesema mchezo huo utakuwa muhimu kwa ajili ya kujipima nguvu na maandalizi ya fainali za kombe la Mataifa ya Afrika zitakazopigwa Afrika Kusini mwaka 2013.

Nematandani ameisifu timu ya Harambee Stars na kusema kuwa ni timu nzuri na watacheza mechi hiyo kwa umakini mkubwa kwa kuwa wanaiheshimu timu hiyo ya Kenya na si timu ya kubezwa.

Mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki utakaochezwa Jumanne Oktoba 16 unasubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa soka jijini Nairobi.

Rais Huyo wa SAFA amesema kuwa wao shirikisho la soka wanavutiwa na mchezo huo kwani Kenya imekuwa ikionyesha nia ya kucheza na Bafana Bafana na hivyo ni muhimu kufanya hivyo.

Timu hiyo ya Bafana Bafana itawasili nchini mwake ikitokea Mjini Warsaw nchini Poland lakini rais huyo hataambatana na timu hiyo kwa sababu atakua akishiriki katika mazishi ya mchezaji wa soka mwenye umri wa miaka 16, Andani Kutama alizimia kwa dakika 13 kabla ya kufariki katika mashindano ya SASFA U-16 Cup.