CECAFA-UGANDA

Kenya, Uganda zatinga hatua ya nusu fainali michuano ya CECAFA, sasa ni kati ya Zanzibar vs Kenya, Tanzania vs Uganda

Hamis Kiiza mchezaji wa Uganda Cranes alikuruka kwanja la mchezaji wa Ethiopia kwenye mchezo wa robo fainali michuano ya CECAFA siku ya jumanne
Hamis Kiiza mchezaji wa Uganda Cranes alikuruka kwanja la mchezaji wa Ethiopia kwenye mchezo wa robo fainali michuano ya CECAFA siku ya jumanne RFI

Timu ya taifa ya mpira wa miguu ya Uganda "The Cranes" na ile ya Kenya "Harambee Stars" zimefanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya kombe la Tusker Chalenji inayotimua vumbi mjini Kampala Uganda.

Matangazo ya kibiashara

Mchezo wa awali uliwakutanisha timu ya taifa ya Kenya ambayo ilikuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Malawi "The Flames" kwenye mchezo ambao Kenya walifanikiwa kuchomoza na ushindi wa bao 1-0.

Kenya walianza mchezo huo kwa kasi na kufanikiwa kupata bao kwa njia ya faulo ambayo iliunganishwa vema na mkongwe Mike Baraza.

Mchezo wa pili uliwakutanisha wenyeji Uganda ambao walikuwa na kibarua dhidi ya Ethiopia kwenye mchezo ambao licha ya Ethiopia kucheza vizuri lakini walijikuta wakipoteza kwa kufungwa 2-0.

Kwa matokeo hayo sasa Uganda watacheza na timu ya taifa ya Tanzania Bara kwenye mchezo wa nusu fainali wakato Kenya wenyewe watakuwa na kibarua dhidi ya timu ya taifa ya Zanzibar.

Mechi kati ya Uganda na Tanzania inatarajiwa kuwa ya kukata na shoka kutokana na upinzani ambao meanza kujitokeza hivi karibuni kati ya timu hizo mbili lakini kwa mujibu wa historia Uganda imekuwa ikifanya vizuri dhidi ya Tanzania.

Kwa upande wa Zanzibar na Kenya mechi hiyo pia inatabiriwa kuwa ngumu kwa timu zote mbili ingawa Zanzibar Heroes wanapewa nafasi kubwa ya kuweza kuibuka na ushindi ingawa mchezo ni dakika tisini.

Nusu fainali hizi zitapigwa siku ya alhamisi ya tarehe 6 mwezi 12 mwaka huu.