SOKA

Chelsea kumenyana na Corinthians katika fainali ya kombe la dunia

Chelsea ya Uingereza itamenyana na Corinthians ya Brazil katika fainali ya kuwania taji la soka la klabu bora duniani baada ya kuifunga Monterrey ya Mexico mabao 3 kwa 1 katika nusu fainali iliyochezwa siku ya Alhamisi nchini Japan.

Matangazo ya kibiashara

Chelsea ambao ni mabingwa watetezi wa taji la klabu bingwa barani Ulaya licha ya kubanduliwa nje ya michuano hiyo msimu huu, walionesha kiwango cha juu wakati wa mchezo wa nusu fainali huku wakimiliki mchezo huo.

 

Mabao ya Chelsea yalitiwa kimyani na Fernando Torres, Juan Mata na Chevez huku Monterrey ikipata bao lake la  kufutia machozi katika dakika za nyongeza kupitia mshambulizi wake De Nigris.

Chelsea inapewa nafasi kubwa ya kushinda taji hilo la dunia ili kujiondolea aibu ya kushindwa kuendelea katika mashindano ya kuwania taji la klabu bingwa barani Ulaya.

Kwingineko, kocha wa klabu ya Corinthians Tite, amekiri kuwa vijana wake walikuwa na wakati mgumu dhidi ya Al Ahly ya Misri licha ya kuwafunga bao 1 kwa 0 siku ya Jumatano katika mchuano wa nusu fainali ya kwanza.

Al Ahly sasa itamenyana na Monterrey kutafuta mshindi wa tatu siku ya Jumapili kabla ya mchuano wa fainali.

Mwaka uliopita Barcelona ya Uhispani ilishinda taji hilo baada ya kuichabanga Santos ya Brazil mabao 4 kwa 0 katika mchuano wa fainali .