SOKA

Wenger kupewa fedha kuwasajili wachezaji wapya Arsenal

Kocha wa klabu ya soka ya Uingereza Arsenal, Arsene Wenger atapata fedha  za kutosha kumwezesha kuwasajili wachezaji wapya wakati wa dirisha dogo la usajili mwezi Januari mwaka ujao.

Matangazo ya kibiashara

Hatua hiyo imefikiwa na viongozi wa klabu hiyo kutokana na matokeo mabaya katika siku za hivi karibuni yaliyooneshwa na timu hiyo ikiwemo ligi kuu ya soka nchini Uingereza .

Mashabiki wa klabu hiyo nchini Uingereza wamekuwa wakitaka maelezo kutoka kwa kocha Wenger ni kwanini hajawasajili wachezaji bora malalamishi waliyoyafikisha kwa viongozi wakuu wa klabu hiyo.

Klabu ya Arsenal imekuwa ikikosa mataji tangu mwaka 2005 waliposhinda taji la shirikisho la soka nchini Uingereza FA na wapenzi wa klabu hiyo pia wamekuwa wakikosoa hatua ya kocha kuwauza wachezaji kama Alex Song, Cess Fabrigas ambao sasa wanachezea Barcelona ya Uhispania na Robin Van Persie ambaye kwa sasa anafanya vizuri Manchester United.

Mashabiki wa Arsenal wanaamini kuwa timu yao ambayo kwa sasa inashikilia nafasi ya saba katika msururu wa ligi kuu nchini Uingereza inaweza kufanya vizuri zaidi hata kunyakua taji la msimu huu ikiwa wachezaji wapya watanunuliwa na kikosi cha sasa kufanyiwa marekebisho.