UINGEREZA

Van Persie akiri ana furaha kuwepo Manchester United na akiamini watatwaa taji msimu huu

Mshambuliaji wa Manchester United Robin Van Persie akifunga goli la pili dhidi ya Wigan Athletic
Mshambuliaji wa Manchester United Robin Van Persie akifunga goli la pili dhidi ya Wigan Athletic

Mshambuliaji wa Kimataifa wa Uholanzi anayesukuma gozi katika Klabu ya Manchester United Robin van Persie amekiri anahisi amezungukwa na Mabingwa kwa sasa na ana matumaini ya kushinda taji akiwa Old Trafford.

Matangazo ya kibiashara

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 29 ametoa kauli hiyo baada ya kufunga magoli mawili kati ya manne waliyoshinda Manchester kwenye mchezo wao dhidi ya Wigan mchezo uliopigwa kwenye dimba la DW.

Van Persie ameweka bayana wamekuwa na utaratibu wa kuangalia na kuweka mikakati katika kila mchezo uliombele yao huku wachezaji wote wakionesha ham,u ya kutaka kushinda taji msimu huu.

Mshambuliaji huyo ambaye ameshafunga magoli 19 tangu ajiunge na Manchester United akitokea Arsenal kipindi cha majira ya joto amesema ukizungukwa na watu wenye uchu hivyo basi ni wazi upo na mabingwa.

Van Persie mwenye magoli 16 kwenye Ligi Kuu nchini Uingereza amekiri Manchester United ni timu ya kipekee na amekuwa na furaha sana tangu ajiunge nayo huku kila mchezaji akionesha utayari wa kushirikiana na wenzake.

Mshambuliaji huyo wa Kimataifa wa Uholanzi hajaficha furaha yake kwa kusema wachezaji wenzake wanagahamu umuhimu wa kushinda kila mchezo na ndiyo maana imekuwa rahisi kwake kuweza kufunga magoli.

Kinara huyo wa ufungaji kwenye Ligi Kuu nchini Uingereza hadi sasa amesema washambuliaji wote wa Manchester United wamekuwa na uchu wa kufunga kitu ambacho kimeongeza chachu ya mafanikio yao.

Kauli ya Van Persie inakuja siku moja baada ya Kocha Mkuu wa Manchester City Roberto Mancini kukiri kushindwa kumsajili mshambuliaji huyo kumezorotesha harakati zao za kutetea ubingwa msimu huu.

Kocha wa Manchester United Sir Alex Ferguson ameendelea kusisitiza kikosi chao kinawachezaji mahiri kwa msimu huu akiwemo Robin Van Persie hatua ambayo imewafanya wawe vinara kwenye Ligi Kuu hadi sasa.